NEWS

Wednesday, 17 July 2024

Siasa: Nape aomba radhi kutokana na kauli yake ya ‘ushindi nje ya boksi’



Nape Nnauye
--------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amewaomba radhi wananchi na wapenda demokrasia nchini, kutokana na kauli aliyoitoa kwamba si lazima CCM ishinde kura kwenye boksi, bali kuna njia nyingine zikiwemo alizosema za haramu.

Akizungumza kupitia video aliyorekodi leo Jumatano Julai 17,2024, Nape ameomba radhi wote waliokerwa na kauli yake.

“Nimeuona mjadala kwenye mitandao, lakini kama nilivyosema kauli ile ilikuwa utani lakini naona umekuwa mjadala mrefu wakati huu kwa sababu tunaelekea katika uchaguzi. Nawapa pole ambao wamesumbuliwa na kuteseka na huu mjadala, nawapa pole na naomba radhi, nasisitiza haikuwa serious,” amesema Nape.

Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, alitoa kauli hiyo iliyoibua mjadala juzi Julai 15,2024 usiku, alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi.

Kauli hiyo ya Nape ilipingwa jana Jumanne na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ambaye alisema haitokani na msimamo wa chama hicho tawala.

“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambie hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” alisema Makalla.

Hiyo siyo mara ya kwanza kwa Nape kutoa kauli tata zenye kuzua mjadala latika kipindi cha kuelekea uchaguzi, kwani hata Juni 2015, akiwa ziarani Sengerema alisema “CCM ingeshinda uchaguzi mwaka huo hata kwa bao la mkono”.
Chanzo: Mwananchi Digital

Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages