NEWS

Wednesday, 17 July 2024

Musoma Vijijini wanavyopiga hatua ujenzi shule za sekondari za kata



Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, 
Profesa Sospeter Muhongo.
--------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-----------------------------------------

Jimbo la Musoma Vijijini katika mkoa wa Mara linaundwa na kata 21 zenye vijiji 68 na vitongoji 374.

Pamoja na maendeleo mengine ya kisekta, jimbo hili chini ya uongozi thabiti wa Mbunge Prof Sospeter Muhongo (CCM), linaendelea kupiga hatua kwa upande wa shule za sekondari.

Hadi sasa, jimbo la Musoma Vijijini lina shule za sekondari 28 zinazofanya kazi, zikiwemo 26 za serikali na mbili za binafsi.

Aidha, kwa sasa shule za sekondari mpya sita zinajengwa, kati ya hizo, tatu zinajengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu na michango ya nguvukazi ya wanavijiji, na nyingine tatu zinajengwa kwa michango ya wanavijiji na viongozi wao.

Pia, ujenzi wa shule nyingine sita unatarajiwa kuanza Julai na Agosti 2024 kutokana na michango ya wanavijiji na viongozi wao, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini.

Malengo makuu
Malengo ya ujenzi wa shule za sekondari mpya katika jimbo la Musoma Vijijini, ni kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali mrefu kwenda masomoni na kurudi nyumbani.

Lakini pia, kupunguza mirundikano ya wanafunzi madarasani, na kujitayarisha vizuri kwenye mfumo mpya wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wote watakaomaliza elimu ya msingi wanapata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza.

Hivyo, Mbunge Prof Muhongo ameombwa na wanavijiji na amekubali kushirikiane nao kuanza utekelezaji wa miradi yao ya ujenzi wa sekondari mpya.

Ujenzi sekondari mpya 6
Ujenzi wa sekondari mpya uko katika kijiji cha Chitare, na hii itakuwa sekondari ya pili katika kata ya Makojo yenye vijiji vitatu.

Ujenzi wa sekondari nyingine mpya ni katika kijiji cha Buanga, ambayo itakuwa ya pili katika kata ya Rusoli yenye vijiji vitatu pia.

Ujenzi mwingine wa sekondari mpya ni katika kijiji cha Nyambono, ambayo nayo itakuwa ya pili katika kata ya Nyambono yenye vijiji viwili.

Sekondari nyingine mpya itajengwa katika kijiji cha Kataryo na kufanya ata ya Tegeruka yenye vijiji vitatu kuwa na sekondari mbili.

Vile vile kutakuwa na ujenzi wa sekondari mpya katika kata ya Kiriba, itakayofanya kata hiyo yenye vijiji vitatu kuwa na sekondari tatu.

Ujenzi wa sekondari nyingine mpya umeelekezwa katika kijiji cha Mmahare, ambao utaiwezesha kata ya Etaro yenye vijiji vine kuwa na sekondari tatu.

Sekondari nyingine 6
Shule za sekondari nyingine mpya zipatazo sita zinatarajiwa kujengwa kutokana na fedha zitakazotolewa na Serikali Kuu.

Hata hivyo, wanavijiji wanashawishiwa kuhangia nguvukazi ili kupata miundombinu mingi ya shule hizo katika jimbo la Musoma Vijijini.

Sekondari mpya ya kwanza itajengwa katika kijiji cha Butata, na kuifanya kata ya Bukima yenye vijiji vitatu kuwa na sekondari mbili.

Sekondari ya pili itajengwa katika kijiji cha Kasoma, ambayo itakuwa sekondari ya kwanza ya amali (ufundi) katika jimbo la Musoma Vijijini, na itakuwa sekondari ya nne ndani ya kata ya Nyamrandirira yenye vijiji vitano.

Ikumbukwe pia kwamba katika kijiji cha Kaboni kilichopo kata ya Nyamrandirira, kuna Shule ya Sekondari ya Juu (high school) Kasoma.

Sekondari ya tatu itajengwa katika kijiji cha Kurwaki. Itaitwa Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu David Massamba kumuenzi Hayati Prof Massamba, ambayo itakuwa sekondari ya pili katika kata ya Mugango yenye vijiji vitatu.

Shule ya sekondari mpya ya nne inajengwa katika kijiji cha Muhoji, ambayo itakuwa sekondari ya pili katika kata ya Bugwema yenye vijiji vinne. Michango ya ujenzi huo inatoka kwa wanakijiji na viongozi wao.

Kwa upande wake Serikali imechangia shilingi milioni 75, na mzaliwa wa Muhoji, Maboto amejenga na kukamilisha chumba cha darasa.

Sekondari mpya ya tano inayojengwa katika kijiji cha Nyasaungu itakuwa sekondari ya pili katika kataya Ifulifu yeney vijiji vitatu. Michango ya ujenzi huo inatolewa na wanakijiji na viongozi wao.

Ujenzi wa sekondari mpya ya sita inajengwa katika kijiji cha kisiwa cha Rukuba, na itakuwa sekondari ya tatu katika kata ya Etaro inayoundwa na vijiji vinne. Ujenzi huo unachangiwa na wana-Rukuba na viongozi wao.

Sekondari mpya tatu zinatarajiwa kufunguliwa kwa kuanza kupokea wanafunzi wa kidaro cha kwanza Januari 2025, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, hivi karibuni.

Maabara za sayansi
Ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vitatu vya maabara za masomo ya Sayansi, yaani Kemia, Fizikia na Bailojia unaendelea katika shule za sekondari jimboni humo.

“Huu ni mradi endelevu hadi sekondari zote za kata na binafsi zitakapokamilisha maabara hizo.

“Wana-Musoma Vijijini tuendelee kushirikiana na serikali yetu kuchangia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu jimboni mwetu. Wazaliwa wa Musoma Vijijini waanze na waendelee kujitokeza kuchangia maendeleo ya vijijini kwao.

“Taarifa za shule za msingi, hususani ujenzi wa shule shikizi mpya, na vyumba vipya vya madarasa zitatolewa baadaye.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 inatekelezwa kwa mipangilio mizuri na kwa mafanikio makubwa jimboni mwetu,” inahitimisha sehemu ya taarifa hiyo ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MATA
#Ukweli kwa Weledi

Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages