NEWS

Wednesday, 17 July 2024

HAIPPA PLC inavyoshagihisha uwekezaji Tanzania



Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, CPA Boniface Ndengo.
-------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-----------------------------------------

HAIPPA PLC ni Kampuni ya Umma iliyosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa ajili ya kujenga mtaji wa shilingi bilioni 500.

Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, CPA Boniface Ndengo anasema kwa sasa kampuni hiyo yenye makao makuu Musoma mkoani Mara, inajihusisha na shughuli za uwekezaji na masoko.

Katika mahojiano na Sauti ya Mara mjini Musoma hivi karibuni, Ndengo ambaye pia ni Makamu Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania, alisema hadi sasa wamefanikiwa kuvutia wanahisa 300 na kujenga mtaji wa shilingi milioni 250.

“Mtaji huu umewezesha kujenga soko kubwa la HAIPPA linaloendeshwa kwa njia ya mtandao kuwapa fursa wabunifu, wajasiriamali, watafiti, wahitimu na wafanyabiashara kutambulisha na kutangaza ubunifu, teknolojia, bidhaa, taaluma, biashara na huduma zao kuwafikia watu wengi ndani ya Tanzania, barani Afrika na duniani kote.

“Mafanikio mengine, HAIPPA tumeanzisha benki ya kuongeza uzito wa mifugo mkoani Mara katika wilaya ya Butiama, na mpaka sasa benki hiyo ina ng’ombe 300,” anasema ndengo.

Anabainisha kuwa lengo la benki hiyo ni kuwa na ng’ombe 10,000 kwa mwaka katika matawi yake yatakayoanzishwa sehemu mbalimbali nchini.

Pamoja na Benki ya Mifugo, anasema HAIPPA pia wanayo Akademi ya Biashara inayowapokea vijana wanaotoka vyuoni na shuleni kuwajengea uwezo wa ubunifu ili wajiajiri kupitia fursa za ujasiriamali na biashara.

“Kupitia akademi hii, mpaka sasa HAIPPA tumeshawezesha wahitimu 12 kutoka Chuo cha Maendeleo Buhare, Chuo cha Mipango Vijijini na Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT),” anasema Ndengo.

Ndengo anatumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wahitimu wa vyuo vya ufundi kama vile VETA, NACTE na vyuo vikuu kutumia fursa hiyo ambayo inawapa wepesi wa kurasimisha biashara zao, kupata ajira, masoko na mitaji.

Mafanikio mengine ya HAIPPA PLC kuwa ni kuanzisha Akademi ya Uwekezaji inayowajengea wananchi fursa na uwezo wa kushiriki uwekezaji mkubwa nchini, ambayo mpaka sasa ina wanafunzi 261, wakiwemo 14 wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Ndengo, elimu ya uwekezaji ni muhimu na inayafaa makundi ya wenye ulemavu, vijana, wazazi na watumishi walioajiriwa serikalini na sekta binafsi, ambao wanapenda kuongeza kipato lakini hawana taaluma, au muda wa kufanya biashara.

“Kama kampuni ya ubunifu, tumejipa wajibu wa kubuni miradi mingi kadri inavyowezekana kusaidia kutatua changamoto za kipato, mitaji na masoko,” anafafanua.

Maono ya HAIPPA PLC kwa mujibu wa Ndengo, ni kuwa kampuni kubwa ya uwekezaji nchini na akademi kubwa ya ubunifu na biashara barani Afrika.

Pia HAIPPA PLC na TCCIA Mkoa wa Mara wanaunga mkono maazimio yaliyofikiwa katika Mdahalo wa Mara Bora kwa Uwekezaji na Kuishi ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC). “Tutashiriki kikamilifu kufanikisha ajenda hiyo,” anasema Ndengo.

Mdahalo huo ulifanyika mjini Musoma hivi karibuni, ambapo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Kuhusu Huduma za HAIPPA PLC, CPA Ndengo anasema zinapatikana kidigitali kwa kupiga *149*46*23# au kutembelea tovuti ya kampuni hiyo, yaani www.haippa.net.

“Kwa yeyote anayetaka kutembelea ofisi zetu tupo Musoma, Mwanza na Dar es Salaam, na pia tunao mawakala mikoa mbalimbali. Kwa mawasiliano zaidi tupigie 0755-947 943,” anasema Mkurugenzi Mkuu huyo wa HAIPPA PLC.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages