NEWS

Wednesday, 17 July 2024

Waridi wa BBC: Rushwa ya ngono inazima ndoto za wasichana wengi




“Safari yangu kama msichana wa Kitanzania ninafahamu umaskini unavyozima ndoto za wasichana.

“Kati ya wanafunzi 200 waliohitimu na mimi kidato cha nne, ni tisa tu ndio tulifaulu kuendelea na masomo ya kidato cha tano, ambapo wasichana tulikuwa watatu pekee.

“Matokeo hayo yaliniumiza sana kuona kwanini wenzangu wengi hawakuweza kufanya vizuri mitihani yao na wengi maisha yao yakaishia mtaani, lakini nikagundua kwamba mazingira hayakuwa wezeshi na bado hata sisi tulikuwa na kazi nzito ya kuhakikisha tunafanya vizuri huko tunakoendelea.”

Lydia Charles Moyo (31), ni mmoja wa washindi sita waliopata tuzo ya shirika la kimataifa la Global Citizen mwaka 2024, kutokana na kuonesha juhudi za vijana duniani katika kuleta mabadiliko na vile vile kutunukiwa tuzo yenye thamani kubwa barani Afrika ya KBF.

Anasema wakati anahojiwa na Global Citizen kuwashawishi kwanini anastahili tuzo hiyo, alitumia simulizi yake kuwaeleza namna alivyokuwa katika hali duni na kuwa na chachu ya mabadiliko katika jamii yake.

Global Citizen ni Shirika la Utetezi na Uhamasishaji la Kimataifa linalopigania kumaliza umaskini.

“...Kupata tuzo hii inabidi wadau duniani wakupendekeze ndiyo ufae, sijui nani alinipendekeza, sikutarajia lakini baadaye katika mchujo kati ya vijana 500 nami nikawa miongoni mwa vijana sita waliopata tuzo,” anasema Lydia.
LYDIA CHARLES MOYO

Tuzo ya pili ni mchakato ambao ulianza Februari 2023, taasisi mbalimbali zilituma maombi ambapo zaidi ya 400 ziliomba na kuchujwa hadi kubaki 25 ambazo zilitakiwa kutuma video ya dakika mbili ya kuelezea kila kitu ili wafanye maamuzi kutoka katika video hizo.

Lydia kupitia taasisi yake ya @herinitiative ameshinda tuzo ya thamani kubwa ya KBF Africa ya Wakfu wa Mfalme Baudouin (King_Baudouin_Foundation) kutokana na kazi zake za uwezeshaji wanawake kiuchumi, ili kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kupambana na ukosefu wa ajira Afrika Mashariki.

Alipokea zaidi ya shilingi milioni 560 za Kitanzania kusaidia wanawake zaidi ya 100,000 kote Afrika Mashariki kufikia ustahimilivu wa kifedha.
LYDIA CHARLES MOYO

Safari yake kitaaluma yenye mabonde na milima
“Masomo na changamoto nilizopitia katika maisha ya kila siku ndivyo vilinipa msukumo nikajikuta nikianzisha hii taasisi ya Her Initiative,” anasimulia Lydia.

“Nilimaliza shule ya msingi nikiwa na ndoto ya kusoma Shule ya Sekondari ya Jangwani, yaani simulizi na taswira niliyokuwa ninaiweka kwenye kichwa changu ni kuvaa sketi ya rangi ya chungwa ya Jangwani.

“Mwaka 2007, matokeo yalipotoka nikabahatika nimechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya kata ambayo wakati huo haikuwa na mazingira rafiki kielimu.

“Kulikuwa hakuna maabara wala madarasa ya kutosha, hakukuwa na walimu wa kutosha, nakumbuka kidato cha pili hatukuwa na mwalimu wa hesabu lakini bado tulifanya mtihani wa taifa,” anaeleza Lydia.

Anasema alikuwa akitamani sana kusoma katika shule maarufu zilizokuwa na mazingira mazuri ya kielimu, lakini hakuwa na namna zaidi ya kuyakabili mazingira magumu ya Shule ya Sekondari ya Kata King'ongo.
LYDIA CHARLES MOYO

Lydia anakiri kuwa aliweka juhudi kubwa sana katika masomo, hasa alipokuwa akiona jitihada za mama yake za kumtaka asome.

Alichaguliwa kusoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Tambaza, ndipo hapo alianza harakati za kuelimisha wasichana wenzake kujitambua na kujithamini.

Anasema alizunguka katika shule mbalimbali kutoa elimu na uhamasishaji, hasa kwa wasichana ili wajitambue na kupata ujasiri wa kuzikabili changamoto zao.

Alianza kuwatafuta wasichana na wanawake maarufu ambao kwa wakati huo walikuwa tayari wanafanya mambo chanya kwenye jamii nchini Tanzania.

“Msemo wangu ulikuwa ‘sisi hatuna hela tunaomba tu uje’, na walikuwa wanakuja," anasema Lydia akitabasamu.

“Nilikuwa nawapigia simu kina Nancy Sumari, Jokate Mwegelo na wengineo nao walikuja na kuzungumza na wasichana,” anaeleza.

Baada ya kumaliza kidato cha sita alipata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anasema maisha ya chuo hayakuwa rahisi, ndiyo wakati aliposhuhudia baadhi ya wasichana wakijiingiza katika tabia hatarishi ili kutafuta kipato cha ziada.

“Kama msichana niligundua nina mahitaji mengi kuliko uwezo niliokuwa nao,” anasema.

Akiwa chuoni, msukumo wa kuanzisha tamasha la ujasiriamali chuoni hapo lililoitwa Panda, kwa maana ya kupanda mbegu ya kujitegemea.

Ni tamasha ambalo aliwaalika wajasiriamali wakubwa Tanzania kuzungumza na wasichana. Wakiwapa wasichana wa vyuoni nafasi ya kuonesha biashara zao, au mawazo yao ya ubunifu wakati huo huo, akijipatia ufadhili ambao ulimwezesha kujikimu.

Anasema amelelewa na mama peke yake, ambaye alikuwa mtumishi wa hali ya chini wa serikali ambaye alisoma mpaka darasa la saba tu.

Mama yake hakuelewa nini hasa Lydia alichokuwa akifanya lakini hakuacha kumuuliza na kumtia moyo.
LYDIA CHARLES MOYO

Harakati kiuchumi zilizogeuza tamasha kuwa taasisi
“Panda ni safari ya msichana wa Kitanzania kujikwamua kiuchumi,” anaeleza Lydia.

Mwanzoni ilianza kama tamasha la kuonesha wazo ujuzi, au biashara za wanawake lakini baadaye aliamua kuifanya kuwa taasisi ambayo inasaidia wasichana kutengeneza kipato, kuanzisha biashara kuzikuza na kupata rasilimali ili kukuza biashara zao zaidi.

“Mwaka 2021, baada ya UVIKO-19 tukajifunza mabadiliko yaliyotokea kote ulimwenguni ili kutunza afya zetu, tuliamua kutengeneza jukwaa la kidijitali la wasichana ili kukutana nao mtandaoni badala ya ana kwa ana,” anasema Lydia.

Jukwaa la Panda dijitali liko katika lugha ya Kiswahili kwa ajili ya wasichana wa Kitanzania kupata elimu na fursa za kibiashara.

Mfumo mseto umetumika kwenye Panda dijitali ili kukidhi mahitaji ya msichana aliyeko kijijini na mjini.

Lidya anafurahia kwamba wasichana wanapata fursa ya kujisajili na kupata fursa mbalimbali, ikiwemo kukutana na wataalamu.

Panda dijitali hii inatoa huduma bure ili kuwezesha wasichana wa kila tabaka kupata fursa na kuitumia ambapo hadi sasa zaidi ya wasicha 6,000 wanaitumia na idadi kubwa ni kutoka vijijini.

Baada ya kupitia changamoto za kimfumo katika kuimarisha taasisi, Lydia aliandika barua kwa wadau wa maendeleo na kuwataka kutowaita tena kama hawako tayari kuwafadhili kukuza ndoto hizi.

Umuhimu wa kustahimili maneno ya kukatisha tamaa

LYDIA CHARLES MOYO

Utamaduni unamzuia msichana kufika mbali. Kila siku msichana anapaswa kufungua masanduku ambayo tamaduni mbaya zimewafungia.

Rushwa ya ngono ni changamoto kubwa sana ambayo inazima ndoto za wasichana.

“Sijui kama inawakuta wavulana lakini kwa wasichana ni tatizo kubwa. Inahitaji uwe jasiri na ujue mifumo ya kuripoti,” anasema.

Lidya anashukuru taasisi yake ambayo inashirikiana na wadau muhimu wa kupambana na rushwa ya ngono na kutengeneza mifumo ambayo inalinda utu wa msichana.

“Changamoto hii imenifanya niwe tayari kukabiliana na lolote, yaani siku hizi ninalipenda zaidi jibu la "NO" HAPANA… kuliko NDIYO.”

“Suala la rushwa ya ngono limekuwa kikwazo kwa wasichana wengi kufikia ndoto zao.

“Nimewahi kukutana na changamoto hiyo sikujua kama ningeweza kuripoti kwa kuwa bado sikuwa na elimu ya kutosha ya kukabiliana na rushwa ya ngono.

“Sikujua namna ambavyo ningeweza kuripoti kujipanga na kukusanya Ushahidi,” anasisitiza.

Ndoto ya baadaye ya Lydia Charles

LYDIA CHARLES MOYO

Anasema ndoto yake kubwa ni kuweza kufadhili wasichana wenye ndoto kubwa.

“Kuna masuluhisho mengi ya changamoto za jamii, lakini wasichana wanakosa fedha ili kufanya hivyo.”

Lydia anasema moja ya vitu ambavyo amejifunza ni kuamini ndoto yake binafsi kabla ya kutegemea wengine wamuamini.

Anasema wasichana wasichoke kugonga milango mingi ipo itakayofunguka.

Kwa wale waliolelewa na mzazi mmoja, Lydia anawataka kuachana na fikra hasi.

Ni vizuri kulelewa na wazazi wote lakini kama imetokea basi wasichana waendelee kufungua masanduku kwamba haijalishi mzazi mmoja, au umelelewa kijijini kila kitu kinawezekana.
Chanzo: BBC
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages