
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (wa sita kulia), Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota (wa sita kushoto), Meneja Mkuu wa Grumeti Fund (wa tano kulia) na viongozi wengine wakifurahia picha ya pamoja na baadhi ya askari wa uhifadhi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Askari wa Wanyamapori Duniani yaliyoandaliwa na Grumeti Fund wilayani Serengeti jana.
----------------------------------------------------
------------------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi amevitaka vyombo vya usalama kutomvumilia mtu yeyote atakayehusika na kile alichokiita kuharibu hifadhi za wanyamapori.
“Natoa rai kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayechezea hifadhi zetu. Serikali tutaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha hifadhi zetu zipo salama,” alisema RC Mtambi alisema wilayani Serengeti jana.
Kiongozi huyo wa mkoa alikuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Askari wa Wanyamapori Duniani (World Ranger Day - WRD) iliyoandaliwa na Grumeti Fund na kufanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Kutoa Elimu ya Mazingira cha shirika hilo.
RC Mtambi alisisitiza kuwa uhifadhi endelevu wa Mapori ya Akiba ya Ikorongo-Grumeti, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Ikona WMA hauna mbadala.
Hivyo aliwapongeza askari wa uhifadhi wa Ikorongo-Grumeti na Grumeti Fund kwa kazi nzuri wanayofanya kulinda maeneo hayo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Alisema bila askari hao wanyamapori ambao ni vivutio vikubwa vya utalii wakiwemo nyumbu wanaohama wanawezea kupotea na kulisababishia taifa hasara.
Aliongeza kuwa uhifadhi wa wanyamapori katika maeneo hayo ni muhimu kwa kuwa unaliingia Taifa mapato zikiwemo fedha za kigeni.
Aidha, RC Mtambi alitoa onyo kali didhi ya vitendo vya uharibifu wa mazingira ya mto Rubana ambao ni sehemu muhimu ya ikolojia ya Serengeti.

RC Mtambi akisalimiana na mmoja wa askari wa wanyamapori wakati wa maadhimisho hayo.
-----------------------------------------------
“Mto Rubana ni chanzo muhimu na lazima kilindwe,” alisisitiza na kuzitaka serikali za vijiji vilivyo jirani na mto huo kuanza kuchukua hatua kali didhi ya watu wanaoharibu mazingira ya mto huo.
“Wenyeviti wa serikaliza vijiji wachukue hatua kali kwa wale wanaokata miti kwenye bonde la Mto Rubana,” alielekeza.
RC Mtambi alitumia fursa hiyo pia kumkaribisha Mkuu wa Wilaya mpya wa Serengeti, Kemirembe Lwota na kumuagiza kusimimia ulinzi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
“DC kwanza karibu Serengeti, nakukabidhi Ikorongo-Grumeti Reserves, Hifadhi ya Serengeti, Ikona WMA na mto Robana. Msipepese macho hata kidogo kwa watu wanaochezea maeneo hayo,” RC Mtambi alimuelekeza DC Kemirembe.
Awali, Meneja Mkuu (GM) wa Grumeti Fund, Matt Perry aliwashukuru askari wa wanyamapori kwa kuendelea kulinda wanyamapori katika mapori ya Ikorongo- Grumeti kwa manufaa ya jamii nzima.
“Kwa niaba ya Grumeti Fund na Grumeti Reserves tunasema asante,” alisema Perry na kuhimiza ushirikiano wa wadau kwa uhifadhi endelevu na maendeleo ya wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya uhifadhi.
“Kwa kufanya kazi kwa pamoja tunaweza kuhakikisha uendelevu wa maisha ya binadamu na wanyamapori,” alisema Perry.

GM wa Grumeti Fund, Matt Perry akizungumza katika maadhimisho hayo.
---------------------------------------------
Kwa upande wake Kamanda wa Uhifadhi wa Ikorongo-Grumeti, Namsifu Marwa alimhakikishia RC Mtambi kuwa wataedelea kulinda wanyamapori na mazingira katika mapori hayo ambayo ni makazi ya wanyamapori wa aina mbalimbali, wakiwemo ‘Big Five’.
Kamanda Marwa alisema ushirkiano uliopo kati Grumeti Fund na Ikorongo-Grumeti ni mfano wa kuigwa.
Grumeti Fund ni Shirika lisilo la Kiserikali linalosaidia uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya jamii katika vijiji vilivyo jirani na Mapori ya Akiba ya Ikorongo-Grumeti ambayo ni sehemu ya ikolojia ya Serengeti.
No comments:
Post a Comment