NEWS

Thursday, 1 August 2024

WWF Tanzania, wadau wa Mradi wa USAID wa Uhifadhi Dakio la Mto Mara wajipanga 24/25



Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara unaotekelezwa na WWF Tanzania chini ya ufadhili wa USAID.
-----------------------------------------------

NA CHRISTOPHER GAMAINA
------------------------------------------

Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania limekutana na wadau wake kuandaa mpango kazi wa 2024/2025 wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Mkutano huo wa siku mbili ulifunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Gerald Musabila Kusaya mjini Musoma, Jumatatu iliyopita.


Katika hotuba yake, RAS Kusaya aliwashukuru WWF Tanzania na USAID kwa kushirikiana na serikali miongoni mwa wadau wengine katika juhudi za kulinda uendelevu wa Mto Mara.

“Wadau wote tuendeleze ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huu tukizingatia kuwa uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira ni ustawi wa maisha ya watu,” alisema Kusaya.


Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada
----------------------------------------------------

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara na Mwakilishi wa USAID Tanzania, Mhandisi Boniphace Marwa alisema wataendelea kushirikiana na serikali katika uhifadhi wa mto huo.

“USAID kwa maana ya Serikali ya Marekani ipo, Serikali yetu ya Tanzania ipo, hivyo bado tutaendelea kushirikiana katika utatuzi wa changamoto za uhifadhi wa Mto Mara,” alisema Mhandisi Marwa.


Mhandisi Boniphace Marwa akizungumza katika mkutano huo
-----------------------------------------------

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Wizara ya Maji kutoka Makao Makuu Dodoma, Mhandisi Sereka Maximillian alisema kipaumbele cha wizara ni uhifadhi na usimamizi wa vyanzo vya maji kwa njia shirikishi.

“Kwa kufanya kazi kwa pamoja tutakuwa na rasilimali za maji endelevu,” alisema Mhandisi Sereka.

Awali, Mratibu wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara kutoka WWF Tanzania, Mhandisi Christian Chonya alisema mradi huo ni wa miaka mitatu (Aprili 22 – Aprili 25) na unatekelezwa katika wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama na Musoma mkoani Mara.

Mhandisi Chonya alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo utanufaisha watu 20,000 kupitia uhifadhi wa vyanzo vya maji, wengine 6,000 kupitia uboreshaji wa usambazaji wa maji na 1,230 kupitia mbinu bora za utunzaji wa ardhi na rasilimali za maji.


Kwa mujibu wa Dkt Lawrence Mbwambo kutoka WWF Tanzania, wameweza kushirikiana na wadau husika kuainisha vyanzo vya maji zaidi ya 100 kwa ajili ya kunufaisha watu 20,000 katika eneo la mradi huo.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Mwakilishi wa RAS Mkoa wa Mara, Mhandisi Mwita Chacha alisema dira ya serikali ni kuweka mifumo ya kuondoa umaskini na kuleta maendeleo kwa jamii.

“Ni matumaini yangu kuwa mpango kazi ulioandaliwa utaboresha ubunifu na ufanisi katika utekelezaji wa Mradi huu wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara kwa manufaa ya jamii,” alisema Mhandisi Mwita.


Baadhi ya washiriki wa mkutano huo ni wawakilishi wa jumuiya za watumia maji, vikundi vya kupima afya ya mto, RUWASA na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, miongoni mwa wadau wengine wa mradi huo, wakiwemo kutoka nchini Kenya.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages