NEWS

Wednesday, 4 September 2024

Wapiga kura wapya 491,050 kuandikishwa Mara, Simiyu na Manyara




Na Mwandishi Wetu

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za mkoa wa Manyara utafanyika kwa siku saba kuanzia leo Septemba 4 hadi 10, 2024 ambapo jumla ya wapiga kura wapya 491,050 wanatarajiwa kuandikishwa.

Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na ambayo yanatokana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, wapiga kura 3,391,017 wanatarajiwa kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa hiyo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhan, idadi hiyo inaweza kuongezeka.

“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo Watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura,” alisema Kailima.

Kwenye uboreshaji huo wa Daftari, jumla ya vituo 4,373 vitatumika kuwaandikisha wapiga kura wapya na kuboresha taarifa za walioandikishwa miaka iliyopita.

Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unafanyika ikiwa ni mwendelezo wa shughuli hiyo iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa mkoani Kigoma, Julai 20, 2024 ambapo mzunguko wa kwanza ulijumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.

Baada ya uboreshaji kukamilika kwenye mikoa hiyo, ulifuata mzunguko wa pili kwenye mikoa ya Kagera na Geita, na wa tatu kwenye mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari unajumuisha mkoa wa Mara, baadhi ya halmashauri za mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu, na mkoa wa Simiyu ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages