NEWS

Wednesday, 4 September 2024

Naibu Katibu Mkuu afunga mafunzo ya uongozi kwa maafisa, askari wa uhifadhi




Na Brigitha Kimario, Serengeti

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (Uhifadhi), Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba amefunga mafunzo ya uongozi kwa wahitimu 236, wakiwemo maafisa 159 na askari 77 wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)

Hafla ya kufunga mafunzo hayo ilifanyika Fort Ikoma, Serengeti ikihusisha pia kuwatunuku vyeo wahitimu hao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Wakulyamba aliwapongeza na kuwataka wahitimu hao kuwa viongozi wa mfano na kuyaishi yale yote waliyojifunza.

“Elimu mliyopata tuione ikiwasaidia kutatua changamoto mnazokutana nazo huku mkisimamia nidhamu na uadilifu ili jeshi letu la Uhifadhi liwe la mfano.

“Mkafanye kazi kwa weledi na bidii mkifuata taratibu, kanuni, sheria na miongozo ya jeshi letu huku mkijiepusha na matendo yanayofedhehesha jeshi. Mkazingatie sheria na haki za binadamu,” aliwambia.

Aidha, Kamishna Wakulyamba alimshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kupandishwa vyeo maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi. Pia alimshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kumtuma kumwakilisha katika hafla hiyo.

“Naishukuru wizara na viongozi wangu kunipa fursa ya kukutana na kuongea na maafisa na askari wa Uhifadhi wengi kiasi hiki kwani ni nadra sana kuwapata wengi namna hii kwa wakati mmoja kutokana majukumu mazito ya uhifadhi na utalii mnayofanya,” alisema.


Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa aliwapongeza wahitimu na wakufunzi wa mafunzo hayo na kusisitiza nidhamu na uwajibikaji kwa wahitimu, hususan wanaporudi katika maeneo yao ya kazi.

“Mafunzo mliyoyapata yamewapa ujuzi wa kujieleza, kutafsiri sera na sheria za uhifadhi wa wanyamapori na misitu, kuandaa mijadala na kusimamia mikakati mbalimbali ya kazi za uhifadhi na utalii. Ni imani yangu kuwa mnaondoka hapa mkiwa tofauti na mlivyokuja,” alisema Mwishawa.

Mwishawa alisema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linatambua kuwa mafunzo waliyopata yataongeza tija katika usimamizi wa rasilimali za nchi walizopewa dhamana ya kuzitunza na kuzilinda ili ziendelee kuchangia pato la Taifa.

Mafunzo hayo ya uongozi kwa maafisa na askari yamefanyika kwa awamu mbili yakilenga kuwajengea viongozi uwezo wa kusimamia nidhamu na kuimarisha mila na desturi za kijeshi kwa nadharia na vitendo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages