Waziri George Simbachawene (mwenye skafu) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa wakisalimiana kwa furaha wilayani Serengeti leo Oktoba 3, 2024.
-------------------------------------
Serengeti
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiagiza mamlaka husika wilayani Serengeti kujenga daraja katika mto Nyahende ili kuwaondolea wakazi wa kijiji cha Getarungu usumbufu na hatari ya kusombwa na maji.
"Ndugu wananchi, miwaombe muwe watulivu… natoa agizo kuanzia leo - ifikapo mwaka kesho mwezi wa kwanza ujenzi wa daraja hilo uwe umeanza," ameagiza Waziri Simbachawene wakati wa ziara yake wilayani Serengeti leo Oktoba 3, 2024.
Awali, wakazi wa kijiji cha Getarungu wamewasilisha kero hiyo kwa waziri huyo wakisema ukosefu wa daraja umekuwa ukisababisha baadhi ya wanakijiji kupoteza maisha kwa kusombwa na maji wakati wakivuka mto huo.
Aidha, wananchi hao wameiomba serikali kuwajengea kituo cha afya ili kuwaondolea adha ya kusafiri mwendo wa kilomita nane kwenda kutafuta huduma katika kituo cha afya kilichopo Nyansurura.
Diwani wa Kata ya Nyansurura, Joseph Seronga amemweleza Waziri Simbachawene kwamba kituo cha afya na daraja katika mto Nyahende ni mahitaji ya kipaumbele kwa wakazi wa kijiji cha Getarungu.
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Amsabi Mrimi amesisitiza kuwa ujenzi wa daraja katika mto huo utakuwa na manufaa pia kwa wanafunzi na wajawazito wanaovuka kwenda ng’ambo ya pili kutafuta huduma.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amesema mradi wa zahanati ya Getarungu ni kielelezo cha kutimiza azma ya serikali ya kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala ya mwaka 2020-2025.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mara, Kanali Evans Mtambi ametoa muda wa wiki nane kwa mamlaka husika ujenzi wa nyumba ya mganga wa zahanati hiyo uwe umekamilika, huku akiahidi kurudi kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Waziri Simbachawene azindua shule mpya iliyogharimu milioni 640/- Butiama, Sagini amshukuru Rais Samia
>>Tragedy on lake Kivu as ferry capsizes, claiming 78 lives
>>Rais wa Barrick akabidhi shule mpya ya kisasa iliyojengwa na mgodi wa North Mara
>>Hospitali ya Halmashauri Musoma Vijijini yaanza kuhudumia wananchi
No comments:
Post a Comment