NEWS

Thursday, 3 October 2024

Waziri Simbachawene akagua miradi ya elimu, maji Tarime



Waziri George Simbachawene (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali mara baada ya kuweka jiwe la msingi Shule mpya ya Msingi Komote katika Halmashauri ya Mji wa Tarime jana.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Tarime

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene jana Oktoba 2, 2024 alikagua na kuweka mawe ya msingi miradi miwili mipya - ya elimu na maji katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Miradi hiyo ni Shule ya Msingi Komote iliyopo kata ya Nkemde katika Halmashauri ya Mji wa Tarime uliogharimu shilingi zaidi ya milioni 500 na ule wa maji Kemakorete unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya shilingi milioni 488,000.


Aidha, akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Kemakorere jioni, Waziri Simbachawene aliwahimiza wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi ujao wa viongozi wa serikali za mitaa.

“Baada ya kujiandikisha hakikisheni pia mnajitokeza kwa wingi kupiga kura za kuchagua viongozi wapenda maendeleo, vinginevyo mtachaguliwa viongozi wapinga maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mara, Kanali Evans Mtambi alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan - mkoa huo umepokea kutoka serikalini shilingi trilioni moja na bilioni 220 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kupitia kwa Waziri Simbachawene kuajiri walimu wengi wakiwemo wale wanaojitolea, hususan wa masomo ya sayansi ili kuzipunguzia shule za mkoani humo changamoto ya wanataaluma hao.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages