
Kikosi cha Timu ya North Mara
Na Mwandishi Maalumu
TIMU ya mpira wa miguu ya North Mara iliichapa Biashara United Veterani mabao 2-1 katika mchezo mkali wa kirafiki uliokuwa wa vuta-nikuvute baina ya timu hizo mbili.
Mechi hiyo ilichezwa Novemba 16, mwaka huu Nyamongo wilayani Tarime ambapo North Mara ilionesha ufundi mkubwa wa kutandaza kandanda safi iliovutia mashabiki walioshuhudia mchuano huo.
Tangu dakika ya kwanza mwamuzi alipopuliza kipenga cha kuanzisha pambano, North Mara ilianza kwa kuwashambulia wapinzani wao lakini ngome ya Biashara United Veterani ilikaa imara.
Baadaye ngome ya Biashara ilionesha kuelemewa kutokana na kushambuliwa mara kwa mara, hivyo hadi dakika za 90 mchuano huo zinamalizika, North Mara iliondoka uwanjani kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1.
Katika mchezo mwingine uliofanyika kesho yake Novemba 17, timu hizo mbili ziligawana pointi baada ya kutoka sare kwa mabao 4-4.
Mchezo huo ulitawaliwa na ufundi zaidi ambapo wachezaji wa timu zote mbili walionesha umahiri wa kusakata kandanda na mashambulizi ya kushtukiza yaliyozaa mabao hayo manne kwa kila upande.

Baadhi ya wachezaji wa Biashara United Veterani.
Baada ya michezo hiyo, Nahodha wa North Mara, Claudy Mugura alisema matukio kama hayo yanavuka mipaka ya mpira wa miguu kwa vile yanajenga ‘madaraja’ na kuimarisha umoja.
"Ni matumaini yangu tutaendelea kuandaa na kufurahia michezo kama hii siku za usoni ili kuimarisha uhusiano wetu sehemu za kazi na katika jamii," alisema Mugura.
Michezo kama hiyo ni jitihada madhubuti zinazofanywa na Kampuni ya Barrick katika kujenga na kuimarisha uhusiano na jamii kwenye maeneo inakotekeleza miradi yake ya uchimbaji madini.
Kampuni ya Barrick inaendesha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
No comments:
Post a Comment