NEWS

Tuesday, 10 December 2024

Mjumbe Baraza Kuu UVCCM Taifa Paul Mwikwabe aanza ziara Mara, akabidhi vizibao kwa bodaboda Musoma Vijijini



Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Dkt Paul Thomas Mwikwabe (kushoto) akisaini kitabu cha wageni Musoma Vijijini alikoanzia ziara yake leo Desemba 10, 2024.
--------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa anayewakilisha Mkoa wa Mara, Dkt Paul Thomas Mwikwabe, leo Desemba 10, 2024 ameanza ziara ya siku nne katika mkoa huo.

Pamoja na mambo mengine, Dkt Paul amegawa msaada wa vizibao (reflectors) kwa baadhi ya waendesha pikikiki za abiria (bodaboda) waliopo Suguti, Musoma Vijijini.


Dkt Paul amepanga kufanya ziara hiyo hadi 13, 2024 Musoma Vijijini, Bunda, Musoma Mjini, Butiama, Rorya, Tarime na kuhitimisha wilayani Serengeti kwa kuhutubia mkutano wa hadhara.

Ameiambia Mara Online News kwa simu leo kwamba lengo la ziara yake hiyo ni kuhamasisha uhai wa jumuiya ya UVCCM katika wilaya zote za mkoa wa Mara.

Amesema atatumia fursa hiyo kukutana na kuzungumza na vikundi vya vijana vinavyonufaika na mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri za miji na wilaya zao, kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025, na vilevile, atakutana na kuzungumza na waendesha 'bodaboda' na mama lishe katika wilaya hizo.

Pia, atawapongeza na kuwashukuru vijana kwa kushiriki na kukipatia chama tawala - CCM ushindi mkubwa katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchini kote Novemba 27, 2024.

“Nitatumia ziara hiyo pia kuhamasisha vijana kuhusu umuhimu wa kujipanga kisiasa kwa ajili ya katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Mwaka 2025,” ameongeza Dkt Paul.

Aidha, katika mikutano yake, Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa atasisitiza umuhimu wa vijana kuweka mipango mikakati ya kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushinda katika chaguzi na kuchochea maendeleo ya mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.

Ziara hiyo inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya kukiimarisha chama hicho tawala na kuhamasisha ushirikiano wa pamoja kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani Mara.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages