NEWS

Tuesday, 13 August 2024

Rais Samia abariki safari ya wakulima kufaidi matunda ya uchumi jumuishi



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mojawapo ya matrekta yaliyozinduliwa wakati wa kilele cha Maonesho ya Nane Nane 2024, kwenye viwanja vya Nane Nane, Nzuguni jijini Dodoma wiki iliyopita.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------

Kuelekea ujenzi wa uchumi jumuishi na endelevu unaolenga kunufaisha mamilioni ya wakulima nchini Tanzania, serikali imekuja na mbinu mahsusi ya kuongeza bajeti, maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbolea, usambazaji wa mbegu bora, uimarishaji huduma za ugani na uwekezaji katika miundombinu.

Nia ya Serikali, kwa mujibu wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ni kuziwezesha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na kuwatajirisha wakulima waliojiajiri kwenye sekta hizo muhimu.

Kwa miongo mingi, sekta ya kilimo ambayo kwa asilimia 75 ndiyo mwajiri mkubwa wa Watanzania, imekuwa ikipangiwa bajeti finyu katika utekelezaji wa shughuli zake.

Hata hivyo, chini ya uongozi wa Rais Samia bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake.

Kwa mfano, kuanzia mwaka 2021/2022 bajeti ya wizara ilikuwa shilingi bilioni 294 ambayo sasa imepanda hadi shilingi trilioni 1.3 kwa mwaka 2024/2025.

Kwa kutoa kipaumble katika uendelezaji wa sekta ya kilimo, juhudi za Rais Samia zimeongeza hamasa kwa wadau wa kilimo kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Katika kuhakikisha kwamba wafugaji na wavuvi wananufaika na uwekezaji na azma ya serikali ya kuwaondoa kwenye umaskini, Rais Samia amesema serikali itajenga na kukarabati viwanda vya mazao ya mifugo na kujenga miundombinu ya uvivi.

Lengo la serikali, kulingana na Rais Samia wakati akihutubia kwenye kilele cha Maonesho ya NaneNane jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, ni kuwasaidia wafugaji na wavuvi kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka vyombo vya fedha ili kuendeleza shughuli zao.

“Lengo la kujenga uchumi jumuishi ni kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na kupunguza umaskini wa kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kutumia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kutengeneza ajira,” alieleza Rais Samia.

Mwaka 2024/2025, Wizara ya Kilimo imepanga kuanzisha vituo 10 jumuishi vya kuhifadhi na kutoa huduma ya zana za kilimo kwa wakulima katika mikoa ya Dodoma, Njombe, Rukwa Mwanza, Mara, Iringa, Katavi, Singida, Manyara na Mbeya.

Nayo Wizaa ya Mifugo na Uvuvi imechukua hatua kadhaa za kuongeza ukubwa wa soko la nyama na samaki ndani na nje ya nchi, zikiwemo ufugaji wa kisasa wenye faida zaidi kwa wafugaji kwa kuongeza malisho kwa wanyama na samaki.

Kwa sasa, mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa ni asilimia saba na sekta ya uvuvi ni asilimia 1.8, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zenye mifugo mingi - ikiwa ni ya tatu baada ya Sudan na Ethiopia kwa kuwa na mifugo zaidi ya milioni 15.
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages