
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji (katikati) na viongozi wengine wakifurahia makabidhiano ya mitambo ya kuboresha barabara katika Hiafadhi ya Taifa Serengeti jana.
----------------------------------------------
-----------------------------------------
Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) jana lilikabidhi msaada wa magreda mawili na mtambo wa kushindilia udongo kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Msaada huo ulikabidhiwa kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Nassoro Kuji.
Mitambo hiyo itasaidia kuboresha mtandao wa barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii nchini.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika Fort Ikoma, magharibi mwa hifadhi hiyo mkoani Mara.
“Tusherehekee na kufurahi kwa kuwapigia makofi FZS kwa mradi wa ERB (Emergency Recovery Support) kutupatia vifaa hivi vya kazi kusukuma gurudumu la maendeleo la Hifadhi ya Taifa Serengeti na TANAPA kwa ujumla,” alisema Kamishna Kuji wakati wa makabidhiano ya mitambo hiyo.
Alisisitiza matumizi mazuri ya mitambo hiyo akisema “Kupokea ni suala moja na matumizi ni suala lingine. Nipende kuahidi kwamba mitambo hii itatumika kama ilivyokusudiwa.”
Kamishna Kuji alitumia fursa hiyo pia kuishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini maendeleo ya sekta ya utalii.
Mitambo hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 ilikabidhiwa na Mkurugenzi Mkazi wa FZS-Tanzania, Dkt Ezekiel Dembe kwa TANAPA.
Magari ya doria yaliyokarabatiwa.
Hali ilivyokuwa kabla ya ukarabati.
---------------------------------------------
Magari hayo yalifanyiwa ukarabati mkubwa chini ya mradi wa Dharura wa Kuhuisha Bioanui (ERB) na yalipokewa kutoka Hifadhi ya Serengeti mwaka jana yakiwa yameharibika sana baada ya kukabidhi magari mapya ya doria 25 kwenye hifadhi hiyo Desemba 2022.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo katika ofisi za FZS mjini Arusha, Kamishna Kuji alisema magari hayo yatatumika kwa shughuli za uhifadhi katika hifadhi nyingine pia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa maliasili.
Aliliomba Shirika la FZS kuendelea kupanua jitihada zake za uhifadhi ili zinufaishe kwa kiasi kikubwa jamii katika kulinda bioanui.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt Dembe alisema Shirika la FZS limekuwa mbia wa muda mrefu wa TANAPA katika jitihada za kulinda maliasili nchini.

Mkurugenzi Mkazi wa FZS-Tanzania, Dkt Ezekiel Dembe akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitambo ya kuboresha barabara katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
--------------------------------------------
Dkt Dembe alisema magari yaliyokarabatiwa yatagawanywa kwa hifadhi 10 ili kuimarisha shughuli za uhifadhi.
Baadhi ya hifadhi zitakazofaidika na mgawanyo wa magari hayo ni Burigi-Chato, Mto Ugalla, Ibanda-Kyerwa, Kisiwa cha Rubondo, Mahale Hills, Rumanyika-Karagwe, Mkomazi, Serengeti, Ziwa Manyara na Katavi.
FZS ni Shirika la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha masuala ya uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa tariban miaka 60 sasa.
No comments:
Post a Comment