
Sehemu ya maofisa ugani na watendaji wa AMCOS wanaoshiriki mafunzo ya mbinu za kilimo bora cha tumbaku yaliyowezeshwa na WAMACU Ltd.
-------------------------------------------------
---------------------------------------
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimewezesha na kuratibu mafunzo ya kilimo bora cha tumbaku kwa maofisa ugani na watendaji wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) kutoka wilaya zinazolima zao hilo mkoani Mara.
Washiriki kutoka wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya wanahudhuria mafunzo hayo ya siku saba yanayofanyika mjini Tarime.
Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) kuwajengea washiriki hao uelewa juu ya uendeshaji wa kilimo bora cha zao hilo la biashara.
Baada ya hapo maofisa ugani na watendaji wa AMCOS watakwenda kueneza mafunzo hayo kwa wakulima husika katika maeneo wanakotoka.
Hivyo, wamehimizwa kutumia nafasi ya mafunzo hayo vizuri ili kupata uelewa wa mbinu bora za kilimo cha tumbaku na fursa zilizopo katika kilimo hicho.
“Lengo la mafunzo haya ni kuhamasisha kilimo bora cha tumbaku na chenye tija ili kuinua kipato cha mkulima, halmashauri husika na kuiingizia nchi fedha za kigeni,” amesema Mtafiti Eric Zawadi kutoka TORITA.
Kwa mujibu wa Nasibu Salum Ngamba kutoka Kampuni ya Alliance One inayojihusisha na ununuzi wa tumbaku, mafunzo hayo yatawezesha wakulima wa zao hilo kuondoka kwenye kilimo cha mazoea kwenda kilimo biashara chenye tija.
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu amesema washiriki wa mafunzo hayo wana wajibu wa kwenda kusimamia ubora wa zao la tumbaku kuanzia shambani hadi sokoni ili kuliwezesha kupata bei nzuri.
“Mkitoka hapa muende kuhamasisha wakulima zaidi kuitikia kilimo bora cha tumbaku ili kuinua pato lao, sambamba na kuwahimiza kujiunga na vyama vya ushirika waweze kuhudumiwa kwa urahisi,” amesema DC Surumbu wakati akifungua mafunzo hayo leo Agosti 13, 2024.

DC Surumbu akiwasilisha hotuba yake
ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
-----------------------------------------------
Aidha, DC Surumbu amezitaka kamati za kilimo za wilaya kuimarisha vikosi kazi vya kusimamia biashara ya mazao ya kimkakati, likiwemo la tumbaku katika maeneo yao ili kudhibiti utoroshaji wake na upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na ushuru wa mazao.
“Niwaombe Wakurugenzi Watendaji na Wakuu wa Sekta ya Kilimo katika maeneo yanayozalisha tumbaku na mazao mengine ya kimkakati kujitahidi kutenga bajeti ya kutosha kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao na ukusanyaji wa mapato,” amesema DC Surumbu.
Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye amesema ushirika huo unaunganisha wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kahawa na tumbaku kutoka wilaya za Tarime, Serengeti, Butiama, Rorya na Buchosa.

GM Gisiboye akizungumza
katika mafunzo hayo.
---------------------------------------------
GM Gisiboye amebainisha kuwa lengo la WAMACU ni kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama wake - kwa kuhamasisha, kuongeza na kuimarisha uzalishaji wenye tija, kukusanya, kuhifadhi, kusindika na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi yenye tija kwa wakulima.
“Pia, WAMACU turatibu upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa maslahi ya wakulima, kuimarisha uwezo wa vyama na wanachama katika kutoa huduma zenye tija kwa wakulima, sambamba na kutafuta na kusogeza huduma ya pembejeo za kilimo karibu na wakulima,” ameongeza.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mafunzo hayo ni pamoja na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mara, Lucas Kiondore, Mwenyekiti wa WAMACU Ltd, Momanyi Range na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye.
No comments:
Post a Comment