NEWS

Monday, 26 August 2024

Sven-Goran Eriksson, kocha wa zamani Uingereza aaga dunia


Hayati Sven-Goran Eriksson, Kocha wa zamani wa Tmu ya Taifa Uingereza enzi za uhai

 
Aliyekuwa wakati mmoja Meneja wa Timu ya Soka ya England, Sven-Goran Eriksson amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76.

Eriksson, meneja wa kwanza ambaye si Mwingereza katika timu ya England, aliiongoza Three Lions hadi robo fainali katika michuano mitatu mikuu katika kipindi chake cha miaka mitano kama kocha - kati ya mwaka 2001 na 2006.

Januari, Eriksson alisema alikuwa na "kama mwaka" wa kuishi baada ya kugunduliwa na saratani.

Familia yake ilisema Jumatatu: "Sven-Goran Eriksson ameaga dunia. Baada ya kuugua kwa muda mrefu, SGE alikufa asubuhi nyumbani akiwa amezungukwa na familia."

Raia huyo wa Sweden aliongoza vilabu 12, vikiwemo Manchester City, Leicester, Roma na Lazio, na kushinda mataji 18.

Eriksson pia aliwahi kuzinoa Mexico, Ivory Coast na Ufilipino.

Baada ya kustaafu kama mchezaji akiwa na umri wa miaka 27, Eriksson alianza kazi yake ya ukocha na Degerfors mwaka 1977 kabla ya kujiunga na timu ya Uswidi ya Gothenburg, ambapo alishinda taji la Uswidi, vikombe viwili vya Uswidi na Kombe la UEFA mwaka 1982.

Kisha aliendelea kufurahia vipindi viwili akiwa na wababe wa Ureno Benfica pamoja na kusimamia vilabu vya Italia Roma, Fiorentina, Sampdoria na Lazio - ambapo alishinda mataji saba likiwemo la Serie A, Vikombe viwili vya Italia na Kombe la Washindi wa Kombe la Ulaya.

Baada ya kugunduliwa na maradhi, hayo Eriksson alitumia mwaka mzima kutembelea baadhi ya vilabu vyake vya zamani, ikiwa ni pamoja na Lazio na Sampdoria.

Mnamo Machi, Msweden huyo, shabiki wa muda mrefu wa Liverpool, alisaidia kuongoza timu ya Liverpool Legends ambayo iliishinda timu ya Ajax Legends mabao 4-2 katika uwanja wa Anfield.

Alitoa ujumbe mzito mwishoni mwa filamu yake mpya ya hali halisi 'Sven', ambayo ilitolewa mapema mwezi huu.

Alisema: "Natumai utanikumbuka kama mtu mzuri anayejaribu kufanya kila kitu anachoweza kufanya.

"Usisikitike, tabasamu. Asante kwa kila kitu, makocha, wachezaji, umati wa watu, imekuwa ya ajabu. Jitunze na uangalie maisha yako. Na uishi."
                                                                     Chanzo: BBC
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages