
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi wa (wa nne kutoka kulia) akizindua Matiko Foundation mjini Tarime jana. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo mpya, Esther Matiko ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara akigawa taulo za kike kwa baadhi ya wasichana wa shule. (Picha: Mara Online News)
-----------------------------------------------
Tarime
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mkoa, Esther Matiko amezindua Taasisi ya Matiko (Matiko Foundation - MF) ili kupanua wigo wa kutoa misaada ya kijamii kwa wakazi wa wilaya ya Tarime na Tanzania kwa ujumla.
“Nikiwa na taasisi hii nitafanya vizuri zaidi katika kusaidia jamii ya Tarime na Tanzania kwa ujumla,” Esther alisema katika hafla ya uzinduzi wa taasisi yake hiyo mjini hapa jana.
Alisema suala la uhifadhi wa mazingira litapewa kipaumbele na taasisi hiyo, ambapo pia alitumia fursa hiyo kutoa msaada wa majiko ya gesi 60 kwa shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Esther ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, pia aliupatia Umoja wa Wakuu wa Shule za Tarime msaada wa machine ya kudurufu mitihani yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 12.
“Pia nimekuja na katoni 70 za ‘sanitary pads’ kwa ajili ya wanafunzi wa kike,” aliongeza Esther.
Alisema taasisi hiyo pamoja na mambo mengine, inasadia kutetea haki za watoto ili waweze kufikia ndoto zao kielimu, kutangaza utalii na kuendeleza michezo katika mkoa wa Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alimpongeza Matiko kwa kuanzisha taasisi hiyo.
“Kwa namna pekee nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kupata wazo la kuanzisha asasi hii muhimu katika jamii yetu. Hongera sana,” alisema Kanali Mtambi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Kwa upande wake mfanyabishara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine ameahidi kuipatia Matiko Foundation mchango wa vitabu vya kiada, kwa mujibu wa Mbunge Esther.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Mwenyekiti wa CCM Mara atembelea ofisi ya wilaya ya Tarime
>>Mahusiano Cup yanavyoujenga mgodi wa North Mara kwa jamii
>>HABARI PICHA:Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa na wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Chifu Zulu ya mjini Songea, mkoani Ruvuma, wakiimba wimbo kuhusu matumizi ya kompyuta jana.
No comments:
Post a Comment