
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo akitangaza tarehe ya uandikishaji wapiga kura kwa wadau wa uchaguzi leo.
-------------------------------------------
Tarime
Halmashauri ya Mji wa Tarime, mkoani Mara imetangaza tarehe ya uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Katika taarifa yake kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mjini hapa leo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo amesema uandikishaji huo utafanyika katika mitaa 81 ya halmashauri hiyo kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024 na kwamba vituo husika vitakuwa wazi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Mkurugenzi Gimbana ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wananchi sifa za kuandikishwa kuwa ni pamoja na raia wa Tanzania, wakazi wa mitaa husika na wenye umri wa kuanzia miaka18 na kuendelea.
Aidha, amewaomba viongozi wa dini, mashirika na wadau wote waliohudhuria na ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria mkutano huo kusaidia kuhamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuandikishwa.
"Tutakuwa na siku 10 za uandikishaji, viongozi wa dini na wengine wote tusaidie kulisema hili, hamasisheni akina mama kugombea kujitokeza nafasi mbalimbali kwa maendeleo jamii na taifa," alisema.

Kwa upande wao wadau wa uchaguzi waliohudhuria mkutano huo wameishauri halmashauri hiyo kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu na wazee kupata fursa ya kuandikishwa kwa ajili ya kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wa serikali za mitaa wanaowataka.
"Haki ikitendeka katika masuala ya uchaguzi, amani hutamalaki kwenye jamii,” amesema Bonny Matto ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tuwakomboe Paralegal (TPO) lenye makao yake wilayani Tarime linajishughulisha na masuala ya sheria na utetezi wa haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment