NEWS

Thursday, 26 September 2024

FZS yahitimisha mafunzo kwa vikundi 30 vya COCOBA wilayani Bariadi



Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya COCOBA wilayani Bariadi yaliyotokewa na FZS, akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi, Mhifadhi Abed Mwesigwa kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti jana Septemba 25, 2024.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Bariadi

Viongozi 60 kutoka vikundi 30 vya Benki Hifadhi ya Jamii (Community Conservation Bank - COCOBA) katika wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu wamehitimu mafunzo maalum ya siku tano yaliyoandaliwa na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).

Mafunzo hayo yamefanyika kupitia Mradi wa Maendeleo na Uhifadhi wa Mfumo wa Ikolojia ya Serengeti - Awamu ya Pili (Serengeti Ecosystem Development and Conservation Project - Phase II).

Mradi huo unafadhilwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo iitwayo KfW, na kutekelezwa na FZS kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika wilaya za Tarime, Bunda mkoani Mara na Bariadi mkoani Simiyu - zinazopakana na hifadhi hiyo upande wa magharibi.

Viongozi waliopata mafunzo hayo ni katibu na katibu msaidizi kutoka kila kikundi, na yalifungwa jana Septemba 25, 2024 mjini Bariadi na Mhifadhi Abed Mwesigwa kutoka Idara ya Mahusiano ya Jamii - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

“Wamefundishwa misingi ya COCOBA kupitia mada za biashara ya fedha, kuweka na kukopa, ujasiriamali, elimu ya uhifadhi, masoko, malisho ya mifugo, usimamizi na uendeshaji wa vikundi hivyo,” alisema Beatus Kyaratingo, mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Kampuni ya Agricomm mkoani Arusha.

Kuhusu malisho ya mifugo, mtaalamu huyo wa uwezeshaji wa vikundi ambaye anafanya kazi na TANAPA na FZS alifafanua kuwa makatibu hao wamefundishwa kilimo cha majani aina ya Juncao yenye virutubisho, ili kuiwezesha jamii kupunguza utegemezi wa malisho kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi.


Kupitia mafunzo hayo kwa ujumla, wanachama wa COCOBA wanapata mbinu na ujuzi wa kuanzisha na kuendesha shughuli halali za kujipatia kipato, badala ya kutegemea uwindaji na biashara haramu ya wanyamapori.

“Lengo letu ni kupunguza utegemezi wa wananchi kwenye maliasili ili nao wawe sehemu ya kuzihifadhi kwa kuepuka shughuli zisizo rafiki kwa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira,” alisema Abubakari Munna ambaye ni Afisa Uhifadhi kutoka FZS kwenye ikolojia ya Serengeti.

Munna alitaja shughuli zisizo rafiki kwa uhifadhi kuwa ni ujangili, hasa uwindaji haramu na biashara ya wanyamapori, ukataji miti, kilimo, uchafuzi wa vyanzo vya maji na ulishaji mifugo hifadhini.

“Tunamsukuru Mungu mpango wetu unaendelea vizuri na unasaidia jamii, maana kupitia vikundi vya COCOBA wanachama wanapata fursa ya kukopa fedha kwa ajili ya biashara na huduma za afya na elimu.

“Lazima tuwe na jamii ambayo sio tu inayonufaika na uhifadhi, lakini pia inayochangia kuhifadhi maliasili zetu,” alisisitiza Afisa Uhifadhi huyo.

Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Edimeth Kaaro aliahidi kusimamia vikundi hivyo vya COCOBA, ili viwe endelevu na vyenye tija kwa jamii na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kwa upande wao makatibu waliopata mafunzo hayo alilishukuru Shirika la FZS na kuahidi kupeleka elimu hiyo kwa wanachama wa vikundi vyao, sambamba na kuhamasisha watu wengi kujiunga navyo kwa maendeleo yao na uhifadhi endelevu.

“Tumefundishwa faida nyingi za vikundi vya COCOBA, mwanachama unaweka hisa kisha unakopa fedha kwa ajili ya biashara na kujiongezea kipato. Tutakwenda kuelimisha wenzetu ili tuweze kujikwamua kiuchumi,” alisema Hesha Boniface kutoka kikundi cha Mwanzo Mgumu.

Naye Zakaria Susani Lukonge kutoka kikundi cha Ikungulyaboba alisema mafunzo hayo yatasaidia pia kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika maeneo yao.

Wahitimu wa mafunzo ya COCOBA wilayani Bariadi wakiimba wimbo wa kulishukuru Shirika la FZS na kuhamasisha uhifadhi endelevu.
------------------------------------------

Kwa mujibu wa Afisa Uhifadhi Munna, mafunzo hayo yamehitimisha mpango wao ulioanza Machi 2024 wilayani Tarime, kisha Bunda na hatimaye Bariadi.

Shirika la FZS lilihamasisha uundaji wa vikundi vya COCOBA na kuvipatia mafunzo ya uwandani kwa siku nne, kisha yakafuata hayo ya siku tano kwa makatibu na makatibu wasaidizi wa vikundi hivyo kwa kila wilaya.

“Katika mafunzo haya kwa ujumla tumeweza kuwafikia wanajamii 1,630 wakiwemo wanaume 781 na wanawake 849. Kati wote hao, 603 wako wilayani Tarime, 267 Bunda na 760 Bariadi.

“Katika wilaya ya Tarime mfumo wa COCOBA umeanzishwa katika vijiji 11 na kuunda vikundi 22, wilayani Bunda vikundi ni 14 katika vijiji saba na wilayani Bariadi kuna vikundi 30 katika vijiji 15.

“Vikundi vya Tarime hadi Juni 2024 vilikuwa na mtaji wa shilingi za Kitanzania 44,038,000. Bunda wao wana mtaji wa shilingi 31,112,600 na Bariadi hadi sasa kwa kipindi cha mwezi mmoja vikundi vimeweza kujikusanyia mtaji wa shilingi 12,085,000,” alisema Afisa Uhifadhi Munna kutoka FZS.

FZS ni Shirika la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha shughuli za uhifadhi, huku ikolojia ya Serengeti ikiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa tariban miaka 60 sasa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages