NEWS

Tuesday, 17 September 2024

Nyanungu wamshukuru Nyambari Nyangwine kwa kukumbuka shule ya msingi aliyosoma



Mgeni rasmi na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa darasa la saba wakati wa mahafali yao katika Shule ya Msingi Mangucha wilayani Tarime, Mara jana Septemba 16, 2024.
---------------------------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News
Tarime

Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard amemshukuru aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangwine kwa kukumbuka kuisaidia shule aliyopata elimu ya msingi.

Shule hiyo ni Mangucha iliyopo kata ya Nyanungu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara.

Diwani Tiboche alitoa shukrani hizo jana kwenye Mahafali ya Darasa la Saba ya Shule ya Mangucha kwa mwaka huu 2024, baada ya Nyambari ambaye pia ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini Tanzania kukubali ombi la kuipatia mashine ya photocopy na printer kwa ajili ya kusaidia kuinua taaluma kwa wanafunzi.

“Nyambari ameonesha mfano mzuri kwa wale ambao walisoma katika shule yetu kongwe ya Mangucha,’ alisema diwani huyo kijana kupitia chama tawala - CCM na msomi wa chuo kikuu.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mangucha, Alfred James Makongo alimshukuru Nyambari kwa msaada huo aliouita wa kihistoria katika shule hiyo.

Jumla ya wanafunzi 68 wakiwemo wasicha 33 na wavulana 35 wameshafanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu katika Shule ya Msingi Mangucha iliyoanzishwa mwaka 1957.

Katika risala yao kwa mgeni rasmi, wanafunzi hao waliziomba mamlaka husika kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wanaripoti shuleni bila vikwazo.

Wahitimu wa darasa la saba 
wakifurahia jambo wakati wa mahafali yao.
---------------------------------------

Nyambari ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo aliwakilishwa na CEO wa Mara Online na Gazeti la Sauti ya Mara, Jacob Mugini.

Mugini ambaye pia ni Mweyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara aliwasilisha salamu za Nyambari kwa wahitimu hao, walimu, wazazi na jumuiya yote ya Shule ya Msingi Mangucha.

“Ndugu yenu Nyambari ameniambia niwambie anawasalimia sana, anawapenda na amekubali ombi la shule la kuwapatia mashine ya photocopy na printer. Pia anawatakia wahitimu wote matokea mema ili waweze kufikia ndoto zao kielimu,” alisema Mugini ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.

Mugini akisoma hotuba 
katika mahafali hayo.
--------------------------------------

Pia Nyambari ameahidi kuwapatia vitabu vya kiada na ziada wahitimu wote watakaofaulu kujiunga na elimu ya sekondari.

Mugini aliwakumbusha wakazi wa kata ya Nyanungu umuhimu wa kuwapatia watoto wao nafasi ya kupata elimu bila kubagua, na kujiepusha na mambo yanayoweza kukatisha ndoto za kielimu kwa watoto.

Wanafunzi wakimkabidhi CEO Mugini zawadi ya keki katika mahafali hayo. Kulia ni Diwani wa Kata ya Nyaningu, Tiboche Richard.
----------------------------------------------

Mugini alitumia fursa hiyo pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mazingira rafiki kwa kila mtoto kupata elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

“Zamani nafasi za kusoma elimu ya sekondari hapa ilikuwa ni shida, leo mna Shule ya Sekondari Nyanungu na serikali inawajengea sekondari nyingine katika kijiji jirani cha Kegonga, lakini pia imewajengea shule nyingine mpya ya Getena ambayo imewapunguzia baadhi ya watoto mwendo wa kutembea kuja kusoma hapa Mangucha.

"Kata ya Nyanungu pia ina mradi mkubwa wa maji ya bomba, umeme upo, kazi inaendelea vizuri Nyanungu, mwenye macho haambiwi tazama,” alisema Mugini huku akimpongeza Diwani Tiboche pia kwa kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo ya kisekta katika kata hiyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages