NEWS

Friday, 6 September 2024

RC Mara azindua ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa Nyatwali



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia) na viongozi wengine wakishiriki kukabidhi hundi ya mfano kwa baadhi ya wananchi wanaohamishwa kutoka kata ya Nyatwali wilayani Bunda jana. (Picha na Godfrey Marwa)
-----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Bunda

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi amezindua ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa kutoka kata ya Nyatwali wilayani Bunda.

Malipo hayo yanatolewa na serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Akizindua ulipaji wa fidia hizo katani hapo jana Septemba 5, 2024, RC Mtambi aliwataka wananchi wanaopata malipo hayo kuondoka eneo hilo, na kutumia fedha hizo vizuri kwa maslahi ya familia zao.

“Akili zenu zianze kufikiria jinsi mtakavyopata faida kutokana na utalii, wanaume wenzangu msichukue nyumba ndogo, baki na uliye naye, tunza watoto mkaanze maisha yaliyo bora. Kama familia muweke mikakati ya pamoja namna ya kuzitumia fedha mtakazopokea ili mpate maendeleo.

"Hili ni eneo la mapito ya asili ya wanyama, pia eneo hili linaweza kuwa na manufaa makubwa ya kiutalii hapa Bunda. Ni vyema mkaliona eneo hili la hifadhi kama eneo lenye fursa za kiutalii ambazo baadaye zitawasaidia kama lilivyo eneo maarufu la Kogatende, Serengeti wanapovuka nyumbu.

"Niwatoe wasiwasi, Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za fidia ambapo malipo haya yataambatana na asilimia saba ya ucheleweshwaji wa malipo tokea uthamini ulipofanyika,” RC Mtambi aliwambia wananchi  hao.

Diwani wa Kata ya Nyatwali, Malongo Mashimo  alieleza kufurahishwa na uzinduzi w wa malipo ya fidia kwa wananchi wake.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Robert Maboto alisema wananchi wapewe elimu ya kutosha ya namna zoezi la ulipaji fidia litakavyofanyika.

Kiasi cha shilingi bilioni 45.9 kimetengwa na serikali kwa ajili ya kuwalipa wananchi  3,658 wanaohamishwa kutoka eneo lenye ukubwa wa ekari 14,250.

Serikali inatwaa eneo hilo la Nyatwali kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi hao.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages