Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara,
Patrick Chandi Marwa.
-------------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa ametuma wito kuhamasisha wanachama wa chama hicho na wana-Mara kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Wana-CCM na wana-Mara kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kwenda kuandikishwa na kuboresha taarifa zetu kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kipindi hiki ambacho shughuli hizo zinaendelea katika maeneo yote ya mkoa wetu.
“Viongozi wa CCM wakiwemo mabalozi wa mashina na wenyeviti wa matawi ya chama wasaidie kuhamasisha wanachama na wananchi wenye sifa kushiriki katika uboreshaji wa daftari hilo,” amesema Chandi alipozungumza na Mara Online News kwa njia ya simu leo.
Amesisitiza kuwa kila mwananchi mwenye sifa zinazotakiwa ana haki ya kikatiba ya kujiandikisha katika daftari hilo kwa ajili ya kupiga kura za kuchagua viongozi watakaotetea maslahi ya wote na taifa kwa ujumla.
“Kama kuna changamoto zozote kwenye vituo vya kujiandikisha, wananchi wasisite kutoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika ili zitafutiwe ufumbuzi haraka,” ameongeza Chandi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa chama tawala, kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni hatua muhimu kuelekea kwenye uchaguzi ujao, na kwa maendeleo ya nchi.
Chandi alimalizia kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maandalizi mazuri ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mara ulianza Septemba 4 na utahitimishwa Septemba 10, 2024 ambapo vituo husika vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni. Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>RC Mara aelekeza wanafunzi wote wapatiwe chakula shuleni.Asifu ufaulu kidato cha VI
>>Tragic boarding school fire in Kenya kills 17 pupils
>>Mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto: Shirila la WiLDAF lawajengea walimu uwezo
>>RC Mara azindua ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa Nyatwali
>>Shooting at Georgia high school leaves at least 4 dead
>>Rebecca Cheptegei, mwanariadha wa Uganda, afariki dunia baada ya shambulio la kinyama
No comments:
Post a Comment