NEWS

Sunday, 27 October 2024

Ajenda ya nishati safi ya kupikia na ugumu wa biashara ya mkaa mjini Bukoba



Mwendesha pikipiki akishusha gunia la mkaa katika mtaa wa Rwamishenye mjini Bukoba kwa ajili ya kusambazwa kwa wateja.
--------------------------------------

Na Phinias Bashaya

Kadiri vita dhidi ya majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira inavyokolea, ndivyo biashara ya mkaa inavyozidi kuwa ngumu katika mji wa Bukoba.

Nyuma ya vita hii, kuna visa vya kusikitisha vya waendesha pikipiki wanaopoteza maisha katika barabara kuu inayoingia mjini Bukoba wakati wakisafirisha bidhaa hiyo kwa njia zisizo rasmi.

Vita hii inapata nguvu na washiriki wapya kila siku, kutokana na ukweli kwamba bila nishati safi ya kupikia, hakuna usalama wa chakula unaotakiwa kuanzia kwenye afya ya mimea isiyovuta nishati chafu.

Ugumu wa biashara hii kwa sasa, unaonekana kwa wavunaji, wasafirishaji, wauzaji hadi watumiaji. Kila kundi lina kilio chake kinachotokana na kukolea kwa mbinyo unaobeba ajenda za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Haishangazi kusikia kutoka kwa Sebastian Kagaruki akiwa miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa bidhaa hiyo katika mji huu, aliyeanza kutafakari uwezekano wa kuwa na biashara mbadala.

Eneo lake la biashara lipo mtaa wa Kilimanjaro katani Kashai. Anasema pamoja na vikwazo vya kisheria kuanzia porini hadi bandani, pia anaviona viashiria vya kuporomoka kwa wateja.

"Ukiwa na kibali unafanya biashara bila shida. Siku hizi kuna changamoto nyingi na wateja wanapungua. Siku hizi kuna haya mambo ya gesi yamepunguza wateja wetu, nasikia wataleta hadi gesi ya kupima kuanzia shilingi elfu tano," alisema Kagaruki katika mazungumzo na Mara Online News mjini Bukoba juzi.

Anaongeza kuwa tishio kubwa la biashara yao kwa sasa ni kundi linalohama kwenda kwenye nishati nyingine, akihofu huenda hali ya biashara hiyo itakuwa mbaya zaidi kama wananchi wengi watamudu gharama za gesi.

Vita ya kulinda mazingira, inaandamwa na kivuli cha sheria na sera zinazoleta ukinzani. Mathalani Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998, na Sheria ya Misitu sura namba 323 na kanuni zake, zinatambua shughuli za kuni na mkaa, na bado kuna sheria za utunzaji wa mazingira.

Hofu ya Kagaruki inathibitishwa na baadhi ya wananchi ambao kwa juhudi zao, wameanza kutengeneza mkaa mbadala kama anavyofanya Nadia Said, mkazi wa mtaa wa Kashenye katani Kashai.

Mkazi wa mtaa wa Kashenye mjini Bukoba, Nadia Said akionesha mkaa mbadala aliotengeneza kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. (Picha zote na Phinias Bashaya)
--------------------------------

Kwa zaidi ya miezi tisa sasa, ingawa hana mafunzo rasmi, anatengeneza nishati hiyo kwa kuchanganya chenga za mkaa na udongo wa mfinyanzi na kwake anaona kuna nafuu ya gharama na hatarajii kurejea tena kwenye matumizi ya mkaa.

Ni miongoni mwa matukio mengi ya juhudi za wananchi wanaotaka kuachana na matumizi ya nishati chafu, ingawa kwa sasa ni vigumu kuyapima kwa ukubwa wake kwa njia ya takwimu.

Hata hivyo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (TIRDO), anasema watengenezaji wengi wa mkaa mbadala hawazingatii uzalishaji bora wa bidhaa hiyo.

"Mkaa mbadala unaweza kuokoa mazingira lakini kuna changamoto za malighafi ya utengenezaji wa mkaa mbadala. Uzalishaji bora ni ule unaotokana na mabaki ya mimea rafiki kwa mazingira," anasema Profesa Mtambo.

Anasema utafiti wa TIRDO unaonesha kwamba kutokana na changamoto ya malighafi, watengenezaji wa mkaa mbadala wanatumia mabaki yatokanayo na kuni, ambayo yanatia mkaa usio na ubora wa kuitwa nishati safi ya kupikia.

Juhudi za kudhibiti matumizi ya nishati chafu katika mji wa Bukoba zimekwenda mbali zaidi hadi kuwaita watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ili waibuke na teknolojia ya kudhibiti moshi wa kuni na taka nyingine wakati wa kuvuna senene.

Uvunaji wa senene katika mji huu huenda sambamba na uzalishaji wa moshi mzito ili kuwapunguza kasi na kurahisisha ukamataji wake, ambapo matumizi ya nishati chafu ya kupikia huendelea hadi jikoni.

Miongoni mwa washiriki wa utafiti huu ni Godfrey Baitu ambaye ni Mhandisi wa Kilimo. Anasema bado wako hatua za awali za kukutana na wavunaji na wauzaji na baadaye kubuni teknolojia itakayokuwa rafiki wa mazingira wakati wa uvunaji wa senene - tofauti na ilivyo sasa

Mmoja wa wavunaji wa senene, mkazi wa mtaa wa Nyamkazi, Revina Rwegoshora anashauri watafiti wabuni teknolojia rahisi ambayo wananchi wengi wataweza kumudu kama wanataka kuondoa moshi mzito wakati wa kuvuna senene.

"Hata sisi moshi unatuathiri macho - yanawasha na kuvimba. Kama wanataka kutusaidia watengeneze vifaa ambayo kila mtu ataweza kununua - hii biashara inategemewa na watu wengi wasio na kipato, visiwe vya gharama kubwa," anasema Revina.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uwekezaji Mkoa wa Kagera, Issaya Tendega anasema lengo la Serikali kuita wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni kutaka wananchi wavune senene bila kuzalisha nishati chafu na kupunguza wingi wa mitego ya senene inayotia doa mandhari ya mji.

Hofu ya mtaalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na viuatilifu (TPHPA) yenye makao yake jijini Arusha, anasema hewa chafu inahatarisha usalama wa chakula na huathiri mfumo wa ukuaji wa mimea, hivyo viini lishe vyake haviwezi kuwa bora.

Kwa sharti la kuhifadhi jina lake kutokana na kutokuwa na kibali cha maandishi kutoka kwa mkuu wake wa kazi, anasema nishati chafu huongeza visumbufu na usugu wa viuatilifu, lakini pia hubadili mfumo wa mimea wa kibaiokemikali na kuathiri utengenezaji wa chakula - madhara yanaweza kwenda hadi kwa mlaji.

"Tafiti zinaonesha kuwa kila ongezeko dogo la hewa ukaa, uzalishaji wa mazao hupungua mara dufu, hivyo inaathiri usalama wa chakula, ardhi inapoteza uwezo wa kuzalisha. Pia ni chanzo cha magonjwa ya mfumo wa hewa, tunatakiwa kutumia nishati safi nyumbani na viwandani," anashauri mtaalamu huyo wa afya ya mimea.

Maelezo yake yanaungwa mkono na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024-2034, uliosainiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, na kuchapishwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Unasema moshi utokanao na matumizi ya nishati isiyo safi hubeba gesi zenye sumu pamoja na chembechembe za vumbi zenye viambata vya sumu, ambazo huweza kudhoofisha mfumo wa upumuaji na chanzo cha magonjwa sugu.

"Takriban watu 33,024 hufariki dunia kwa mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa katika makazi. Magonjwa mengi yangeepukwa kama nishat safi ingetumika," inasema sehemu ya mkakati huo.

Pia, Mkakati huo wa Taifa kwa miaka 10 ijayo, unanukuu takwimu za Benki ya Dunia za Mwaka 2023 kwamba idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imeongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021.

Mhifadhi Mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Wilaya ya Bukoba, Anatoli Legwen anasema miti inapokatwa mionzi ya jua hufika moja kwa moja kwenye uso wa dunia bila kupunguzwa makali, na hufyonza hewa ukaa.

Kwamba kuna athari nyingi, na chanzo ni uharibifu wa mazingira unaokaribisha magonjwa ya macho na matatizo kwenye mfumo wa upumuaji, ambapo anasema wanagawa miti ya kupanda bure kama sehemu ya jitihadta zao.

Somo la kutengeneza mkaa mbadala nyumbani ni rahisi. Unahitaji masalia ya mimea na mabaki ya mazao. Hugundishwa kwa kutumia vifungio kama udongo, wanga (unga wa mhogo na viazi vitamu) na molasi au gundi.

Masalia ni kama vile karatasi, vumbi la mbao, majani makavu na pumba za mpunga ambazo ni malighafi zinazoweza kupatikana kwa urahisii bila gharama kubwa.

Mbele ya ajenda hii kuna sauti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote anasisitiza kwamba matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa sasa ni mahitaji ya lazima na sio anasa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages