Na Mwandishi Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan jana alihitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru jijini Mwanza baada ya kukimbizwa nchini kote kwa miezi sita.
Mwenge huo jana ulikabidhiwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ili kupandishwa tena kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya kutimiza miaka 60 tangu Tanzania Bara na Zanzibar zilipoungana Aprili 26, 1964, kuunda Jamhuri ya Muungano.
Rais Samia alitumia fursa hiyo ya kilele cha Mbio za Mwenge kuwahimiza na kuwahamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi ujao, Novemba 27 mwaka huu.
Kaulimbiu ya Mwenge mwaka huu iliweka mkazo kwenye suala nyeti la utunzaji mazingira na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ujenzi wa taifa endelevu baada ya miongo sita tangu kujipatia uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza.
Kabla ya kuhitimisha Mbio za Mwenge kwenye Uwanja wa CCM wa Kirumba jijini Mwanza, Rais Samia alihudhuria misa ya kumbukizi ya robo karne -- miaka 25 -- ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika kanisa Katoliki jijini Mwanza.
Aliwaambia waumini kwamba fikra na falsafa za Mwalimu kuhusu maendeleo zitaendelea kudumishwa kama tunu za taifa zinazomulika mapito ya Watanzania katika maisha yao.
Tunu alizoziacha Mwalimu nchini hazina kipimo -- kuanzia umoja, amani, uadilifu, kupigania haki, kulaani ukatili nchini na duniani, kuwapenda watu wanyonge, kupiga vita uonevu na dhuluma na kulaani unyonyaji unaofanywa na mataifa makubwa kwa nchi changa.
Mwalimu Nyerere alikuwa na mmoja wa viongozi magwiji wa siasa barani Afrika aliyepigana bila kuchoka kushinikiza kupatikana kwa uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika.
Baadhi ya nchi hizo ni Msumbiji, Afrika ya Kusini, Namibia, Angola na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment