Mbunge wa Butiama mkoani Mara na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini (katikati) akiwa kwenye tafrija ya kuwapongeza walimu jimboni humo leo Oktoba 2, 2024.
---------------------------------------------
Butiama
Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Jumanne Sagini ameweka wazi dhamira yake ya kubadilisha Shule ya Sekondari Kiabakari kuwa ya vipaji maalum, sambamba na kuanzisha shule za msingi za mchepuo wa Kiingereza jimboni humo.
Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, amesema lengo la dhamira yake hiyo ni kuinua na kuboresha taaluma katika jimbo hilo iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Ameyasema hayo katika tafrija maalum aliyoandaa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuwapongeza walimu wa shule za sekondari za juu (high schools) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chief Ihunyo High School jimboni humo leo Oktoba 2, 2024.
"Kiabakari tuibadilishe kuwa shule ya wilaya, tuwe tunachukua mwanafunzi bora kwa kila kata, tufanye Kiabakari kuwa 'centre of excellence’.
"Pia, niko tayari kujitolea mwende halmashauri za Dar kujifunza namna ya kuanzisha shule za msingi za English Medium," amesema Sagini.
Aidha, Naibu Waziri Sagini amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dtk Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimkakati inyoendelea kutekelezwa mkoani Mara, ikiwemo ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, miradi ya maji na elimu.
Katika tafrija hiyo, walimu wamekabidhiwa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu, vyeti maalum, pasi za umeme, majiko ya gesi na vitambaa vya nguo ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wao kwenye masuala ya elimu.
Mbunge Sagini (mwenye suti) akimkabidhi mmoja wa walimu zawadi ya jiko la gesi katika tafrija hito.
------------------------------------------
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Aziza Baruti, kupanda kwa taaluma kwa miaka minne mfululizo, yaani mwaka 2021 hadi 2024 katika halmashauri hiyo, ni matokeo ya walimu kufanya kazi kwa uvumilivu na kujituma.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mwalimu Chacha Megewa amemshukuru Mbunge Sagini kwa ushirikiano anaowapa walimu, ikiwa ni pamoja na kuwasemea na kutatua changamoto za kielimu kwa wakati, hali ambayo inaongeza ari kwa watumishi katika halmashauri hiyo alikozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarange Nyerere.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Nyambari achangisha tena shilingi zaidi ya milioni 200 Kanisa Katoliki Nyamwaga, mwenyewe achangia milioni 42/-, Parokia yamkabidhi Askofu Msonganzila gari jipya
>>Waziri Simbachawene akagua miradi ya elimu, maji Tarime
>>Hospitali ya Halmashauri Musoma Vijijini yaanza kuhudumia wananchi
>>Mradi wa Smart City wayeyuka Serengeti, ni ule uliotangazwa kutengewa shilingi trilioni 2
No comments:
Post a Comment