NEWS

Thursday, 17 October 2024

Wananchi Nyatwali: Tunaishukuru Serikali kututua mzigo wa adha za tembo



Wanyamapori aina ya tembo wakiwa Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, mpakani na kata ya Nyatwali wilayani Bunda, kama walivyokutwa na camera ya Mara Online News wiki hii.
------------------------------------------

Na Christopher Gamaina/ Mara Online News

Wananchi katani Nyatwali katika wilaya ya Bunda mkoani Mara wamepokea kwa furaha na matumaini chanya uamuzi wa Serikali wa kuwahamisha baada ya kuwalipa mabilioni ya fedha kufidia mali zao mbalimbali katika eneo hilo.

Hatua hii ya kihistoria sio tu kwa ajili ya upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, bali pia inalenga kuwatua wananchi hao mzigo mkubwa wa adha za wanyamapori waharibifu na wakali.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti katani Nyatwali wiki hii, wananchi hao hawakujizuia kuonesha furaha yao inayoashiria mwanzo mpya wa matumaini na mafanikio.

“Ninaishukuru sana Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia [Dkt Samia Suluhu Hassan] kwa kufanya uamuzi wa busara wa kutuhamisha kutoka hapa Nyatwali ili tuepuke madhara yanayosababishwa na wanyamapori, hasa tembo.

“Tumekuwa tukijizatiti kulima mazao lakini yanamalizwa na tembo mashambani, mtu unajikuta huna kitu, unaishi kwa shida. Kwa kitendo hiki cha kutuhamisha, mimi naona Serikali imetutua mzingo mkubwa,” anasema Mary Wambura anayehama kutoka Nyatwali.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Saida Jilala anafurahia kuhamia Lamadi wilayani Busega katika mkoa wa Mwanza lakini hatasahau magumu aliyopitia katani Nyatwali. “Tembo walibomoa nyumba zangu na kushambulia mashamba yangu mara nyingi,” anasema.

Sylvester Erasto yeye anahamia Manyamanyama, Bunda huku akiwa na kumbukumbu chungu ya jinsi tembo walivyo hatari kwa mazao mashambani na majumbani katika kata ya Nyatwali inayoundwa na mitaa ya Tamao, Kariakoo, Serengeti na Nyatwali.

“Maisha ya hapa Nyatwali watu hawalali usingizi, wanakesha wakilinda mazao mashambani yasiliwe na tembo. Hata ukivuna na kuyahifadhi majumbani tembo wanavunja nyumba na kuyala,” anasema.


Kwa upande wao Ibrahim Shaa na Leah Lamso wanaishukuru Serikali, huku wakiomba wananchi katani Nyatwali waimarishiwe ulinzi pamoja na mazao yao mashambani wakati wakiendelea na maandalizi ya kuhama.

“Tunaishukuru Serikali kwa sababu licha ya kutulipa fidia za mali zetu, imeruhusu tuondoke na tunazoweza kubeba kama vile mabati, mbao na hata matofali. Ila tunaomba ituimarishie ulinzi tembo wasiharibu mazao yetu mashambani wakati huu wa maandalizi ya kuhama,” anasema Shaa.

Mojawapo ya malori yanayotumika kusafirisha mizigo ya wananchi wanaohama Nyatwali.
-------------------------------------------

Mbali na kuharibiwa mazao, wananchi katani Nyatwali pia wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi na hofu ya kujeruhiwa na hata kuuawa na wanyamapori wakiwemo tembo.

Pia, kumekuwepo na matukio ya wakazi wa kata hii kuuawa na mamba wakati wakioga na kuchota maji, lakini pia kuzama na kufa maji wakati wakifanya uvuvi katika Ziwa Victoria.

Aidha, baadhi ya nyumba zimekuwa zikikabiliwa na mafuriko ya ziwa. “Kuna watu nyumba zao zimemezwa kabisa na ziwa hili,” anasema Jumanne Nyanda.

Mitumbwi unayotumika katika shughuli za uvuvi ikiwa ufukweni mwa Ziwa Victoria katani Nyatwali.
--------------------------------------

Naye mfanyabiashara Deo Mgengeli aliyekuwa anamiliki kambi ya kitalii katani Nyatwali ni miongoni mwa wananchi walioridhishwa na taratibu za Serikali katika uhamisho huo.

“Ulipaji fidia umefanyika vizuri, hauna ubabaishaji. Ninaipongeza na kuishukuru Serikali,” anasema Mgengeli ambaye ni wakili mstaafu.

Deo Mgengeli akizungumza na 
wanahabari katani Nyatwali.
--------------------------------------------

Kwa mujibu wa Mthamini Mteule wa Mkoa wa Mara, Ernesto Sanga, watu takriban 4,000 walifanyiwa tathmini ya mali zao mbalimbali zikiwemo nyumba na mashamba kwa ajili ya kulipwa fidia ili kuhama Nyatwali.

“Tumebakiza awamu ya mwisho inayokuja ya kufanya uthaminishaji wa makaburi na mali nyingine za watu ambao hawakujitokeza wakati wa uthaminishaji wa kwanza,” anasema Sanga.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi wanathibitisha kuwa Serikali imeshatoa shilingi bilioni 45.99 za malipo ya awali ya fidia kwa wananchi waliofanyiwa uthaminishaji wa mali zao, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akisisitiza jambo kwa wananchi katani Nyatwali wiki hii. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano.
----------------------------------------------

“Mheshimiwa Rais Dkt Samia alisikia kilio cha wananchi hawa akaamua kuidhinisha fedha zitolewe walipwe fidia waondoke eneo hili ambalo ni hatari kwa maisha yao na mali zao,” anasema Mtambi na kuwashauri wananchi hao kutumia vizuri fedha hizo, ikiwemo katika ujenzi wa makazi mapya kwa manufaa yao na familia zao.

TANAPA wanawalipa wananchi hao fidia hizo kwa njia ya hundi kupitia Benki ya CRDB. Meneja wa Benki hiyo Tawi la Bunda, Marwa Solomon anasema walianza kutoa malipo hayo Oktoba 9, mwaka huu na walitarajia kukamilisha kazi hiyo Oktoba 15, mwaka huu.

Kazi ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa ikiendelea katani Nyatwali.
------------------------------------------

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Andrew Mombo kutoka Makao Makuu ya TANAPA - Arusha anasema eneo la Nyatwali lenye ukubwa wa hekta 14,250 na kilomita za mraba 54.57 sasa litakuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Mombo anaweka wazi kwamba zamani kabla ya watu kuhamia na kuishi, eneo hilo lilikuwa mapito (ushoroba) muhimu ya wanyamapori kutoka Hifadhi ya Serengeti kwenda kunywa maji Ziwa Victoria.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Andrew Mombo akizungumza na waandishi wa habari.
---------------------------------------------

“Ninamshukuru Rais wetu Dkt Samia Sukuhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuhamisha wananchi kutoa eneo hili ambalo ni muhimu kwa uhifadhi wa wanyamapori na ikolojia ya Serengeti, ni uamuzi wa busara na wenye manufaa kwa taifa letu,” anasema Mombo.

Anaongeza kuwa kutwaliwa kwa eneo hilo ambalo linaunganisha Hifadhi ya Serengeti na Ziwa Victoria kutafungua na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, uwekezaji na uchumi katika ukanda huo na mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi anasema eneo la Nyatwali lilinalofahamika pia kama Ghuba ya Speke, litaongeza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 14,763 hadi 14,817.67.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi akizungumza na waandishi wa habari.
----------------------------------------------

Msumi anasema hatua ya kuchukua eneo hilo kwa ajili ya upanuzi wa hifadhi hiyo inayoongoza kwa vivutio na huduma bora za utalii Afrika, itawezesha wanyamapori kupata urahisi wa kwenda kunywa maji Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyatwali, Deaynes Mawora, watu wote 7,022 (wanaume 3,538 na wanawake 3,484) waliokuwa wanaishi katani hapo wanahamishwa pamoja na mifugo (ng’ombe, mbuzi na kondoo) yao zaidi ya 20,000.

“Mwitikio wa watu kuhama ni chanya, waliopokea malipo yao ya fidia wanaendelea kuhama, tunaomba huko wanakohamia wapokewe vizuri,” anasema Mawora.

Ubomoaji wa nyumba kwa ajili ya kuhama unaendelea Nyatwali. (Picha zote na Mara Online News)
------------------------------------------------

Wananchi hao sasa wanakwenda kuanza maisha mapya katika maeneo tofauti ambayo ni salama kwao na mali zao, huku wakiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kutekeleza mchakato huo kwa weledi.

Uhamisho wa wananchi hao kutoka Nyatwali, ni mfano mzuri wa jinsi Serikali inavyoweza kuchukua hatua za haraka na za maana ili kulinda maisha ya watu, wanyamapori na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages