
Na Joseph Maunya, Tarime.



Jamii wilayani Tarime imeombwa kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Wito huo ulitolea hivi karibuni na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play wakati wa tamasha la michezo la kiuhamasishaji kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Tamasha hilo liliandaliwa na taasisi hizo na kufanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Keisangora iliyopo kata ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), likijumuisha pia wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamirema.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi Keisangora na Nyamirema wakifuarahia picha ya pamoja.
Akizungumza katika tamasha hilo, Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisema elimu kwa watoto wa kike ni muhimu kwani inaweza kuwasaidia kupata nafasi kubwa za kiuongozi na kitaalamu siku za mbeleni.
"Nitoe wito kwa kila mtu alieko hapa tukawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwa sababu elimu hiyo itawapa fursa na baadaye tunaweza tukapata viongozi wakubwa kama Rais wetu mama Samia [Dkt Samia Sulihu Hassan]," alisema Fungo.

Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo akisisitiza jambo katika tamasha hilo.
Naye Afisa Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwalimu Alfred Misana aliekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, aliwashukuru AICT na Right to Play kwa kuendelea kutoa hamasa hiyo kwa jamii, huku akieleza faida za kumpatia mtoto wa kike elimu.
"Mimi nawashukuru sana wafadhili wetu [AICT na Right to Play] kwa kuendelea kutuletea matamasha haya kwani yanatoa hamasa kubwa sana na sisi kama jamii tutashiriki kampeni hii kwa sababu tunatambua kwamba ukimuelimisha mtoto wa kike basi umeelimisha jamii nzima," alisema Mwalimu Misana.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Keisangora, Samson Magarya alisema hamasa inayotolewa na taasisi hizo imekuwa chachu kubwa ya mabadiliko, hasa kwa watoto wa kike ambao hivi sasa wanapenda shule tofauti na kipindi cha nyuma.
"Nawashauri wazazi wanaokataza watoto wasije shule wawalete shule wapate elimu kwa sababu elimu itawasaidia ili baadaye nao wasaidie na familia zao kujiendeleza kiuchumi," alisema Grace Manga Msabi, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Keisangora.

Tamasha hilo limehusisha michezo ya mpira wa miguu kwa wavulana na mpira wa Pete kwa wasichana, ambapo washindi wamepewa zawadi ya jezi za mpira na vinywaji baridi kwa wanafunzi wote.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>CHADEMA yashinda vijiji 4 Tarime Vijijini katika kata 3, imo Ganyange
>>RC Mara aongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watu 8 waliokufa kwa mafuriko mto Mori
>>Dkt. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa WHO Kanda ya Afrika, afariki dunia
>>Biteko awatajia wananchi 'viongozi wa maendeleo' akizindua kampeni za CCM Mara
No comments:
Post a Comment