Viongozi wakikabidhi zawadi ya jezi kwa wanafunzi wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT na Right to Play katika Shule ya Msingi Nyamombarawilayani Tarime jana.
Na Joseph Maunya/ Mara Online News
Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimatiafa la Right to Play wametajwa kuongeza ari ya kazi kwa walimu kutokana na misaada mbalimbali wanayopeleka shuleni ambayo imekuwa ikiwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana Novemba 26, 2024 na Afisa Elimu Kata ya Nyanungu, Mwalimu Kimito Petro wakati wa tamasha la michezo la kiuhamasishaji lililoandaliwa na taasisi hizo kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyamombara iliyopo kata ya Nyanungu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamombara wakifurahia picha ya pamoja.
“Niwashukuru [AICT na Right to Play] maana mnapokuja kama hivi mnatuwezesha kwa rasilimali mbalimbali zinazotupatia motisha ya kuendelea na uelimishaji jamii kwa kuwa haya mambo tunayoongelea leo yapo sana katika jamii zetu. Kwa hiyo niwaombe muendelee kuja katika shule zote za kata yetu ya Nyanungu,” alisema Mwalimu Kimito.
Naye Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisema elimu ya umuhimu wa kutoa haki sawa kwa watoto wa kike, ikiwemo haki ya elimu imekuwa ikienezwa kwa jamii ili ibadilike na kuacha vitendo vya ubaguzi wa kijinsia na ukatili kwa watoto.
Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo akizungumza katika tamasha hilo.
“Tunaendelea kutoa elimu hii kwa maana haya mambo yapo katika jamii yetu na ndiyo maana tuko hapa leo ili kuendelea kuielimisha jamii ya maeneo haya na kila mtu anayesikia sauti hii atambue kwamba mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume. Kwa hiyo jamii ibadilike na iachane na mila potofu dhidi ya watoto wa kike,” alisema Fungo.
“Nawaomba AICT na Right to Play waendelee kutuelimisha juu ya umuhimu wa elimu kwetu sisi watoto wa kike, na sisi tukifika majumbani tutaelimisha watu wengine ili waache kuozesha watoto wao katika umri mdogo, na badala yake wawapeleke shule,” alisema Scola Marwa Chacha wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Nyamombara.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Nyamombara, Paschal Magerani Safari alizishukuru taasisi hizo kwa jitihada zao za uelimishaji wa jamii akisema ujumbe huo utafika mbali zaidi kwa kuwa atashiriki kuumbaza kwa jamii na kusaidia watoto wa kike.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>CHADEMA yashinda vijiji 4 Tarime Vijijini katika kata 3, imo Ganyange
>>RC Mara aongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watu 8 waliokufa kwa mafuriko mto Mori
>>Dkt. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa WHO Kanda ya Afrika, afariki dunia
>>Tarime: Watu 9 wafa mafuriko ya mto Mori unaotiririsha maji Ziwa Victoria
No comments:
Post a Comment