NEWS

Thursday, 28 November 2024

RC Mara aongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watu 8 waliokufa kwa mafuriko mto Mori




Na Waandishi Wetu/ Mara Online News

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watu wanane waliokufa kwa kusomba na mafuriko ya mto Mori wilayani Tarime. Mto huo unatiririsha maji kwenye Ziwa Victoria nchini Tanzania.

Tukio la kuaga miili hiyo limefanyika leo Novemba 28, 2024 kwenye viwanja vya Bugosi, kisha kusafirishwa kwenda kuzikwa katika makaburi ya Magena, nje kidogo ya mji wa Tarime.


Mkuu wa Mkoa Kanali Mtambi ametumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wilayani Tarime kuchukua hatua za kuwaondoa haraka watu wanaoishi jirani na mto huo ili kuwaepusha na hatari ya kukumbwa na maafa ya aina hiyo.

"Maeneo ya mabondeni kwenye mikondo ya maji siyo salama kwa maisha yetu, hivyo tusikae maeneo hayo. Tuchukulie majonzi haya kama funzo baya kwa sababu tumepoteza ndugu zetu.

“Niwatake viongozi wote tushirikiane tuhakikishe wananchi wetu wote wanaondoka katika maeneo hayo hatarishi. Tutoe elimu, na kama haipokewi - ikilazimika itumike nguvu kunusuru wenzetu hawa," ameagiza.

Kanali Mtambi akitoa agizo la watu kuondolewa mabondeni.

Wakati huo huo, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umetoa msaada wa dharura uliojumuisha magodoro, vyakula na vifaa vya shule kwa ajili ya familia zilizopoteza wapendwa wao, huku makazi na mali zao vikisombwa na mafuriko hayo ya mto Mori.

Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi na mfanyakazi mwenzake, Christopher hermence wamekabidhi msaada huo kwa familia hizo mbele ya Mkuu wa Mkoa.

Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi (aliyevaa shati la kaki) na mwenzake Christopher Hermence wakikabidhi msaada huo.

"Sisi pia kama mgodi tumeguswa na tukio hili kwa kuwa sisi pia ni sehemu ya jamii. Hivyo kwa niaba ya mgodi tunatoa pole sana kwenu, lakini pia tunatoa msaada wa magodoro matano, mchele, mafuta, sabuni na vifaa vya shule kwa walionusurika katika maafa haya," amesema Uhadi.

Mafuriko hayo ya mto Mori yalitokea Novemba 24, 2024 saa nne usiku katika mtaa wa Bugosi uliopo kata ya Nyamisangura.

Kati ya watu 11 wa familia ya Elias Ngare ni wawili walionusurika katika ajali hiyo ya mafuriko, pamoja na wengine tisa wa familia ya Edward, licha ya kuachwa bila makazi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages