
Na Mwandishi Wetu, Tarime

Kampeni ya Kimataifa ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia imezinduliwa wilayani Tarime, kwa ushirikiano mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Jeshi la Polisi na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, miongoni mwa wadau wengine.
Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo Novemba 25, 2024 kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nyamongo, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele.
Katika hotuba yake, Meja Gowele amewaomba wanajamii wote kushiriki katika mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukiwemo ukeketaji wasichana unaotajwa kukumbatiwa wilayani Tarime.
“Kampeni hii iwe ya kila mtu, isiwe ya taasisi au kampuni fulani pekee, inahitaji nguvu ya pamoja na ushirikiano, kila mmoja aone hili ni tatizo katika jamii,” amesema.
Aidha, amewataka wazee wa mila na ngariba (wakeketaji) kuacha kuhamasisha ukeketaji kwani vyombo vya dola vimejipanga kukamata na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaobainika kukaidi katazo hilo la serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele akizungumza katika uzinduzi huo.
Meja Gowele ametumia nafasi hiyo pia kuushukuru na kuupongeza mgodi wa North Mara akisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika kutatua changamoto za wananchi.
“Mgodi wa North Mara umekuwa mstari wa mbele katika kuhudumia jamii, ninawaomba wananchi tuendelee kuuunga mkono kwa kazi kubwa unayofanya,” amesema kiongozi huyo wa wilaya.
Viongozi wa Serikali na mgodi wa North Mara katika pichaya pamoja na wadau wa kuponga ukatili wa kijinsia wilayani Tarime.
Akitoa salamu zake katika hafla ya uzinduzi huo, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko amesema mgodi huo ni sehemu ya jamii, hivyo una wajibu wa kushirikiana na wadau mbalimbali kupinga vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.
“Sisi kama mgodi kwa upande mmoja tuna wajibu na taratibu za kuheshimu tamaduni, mila na desturi za jamii katika maeneo tunayochimba madini. Lakini kwa upande mwingine tuna wajibu na taratibu za kuheshimu haki za binadamu,” amesema Lyambiko.
Ameongeza kuwa mgodi huo unazingatia umuhimu wa kushirikiana na wadau wengine katika kuelimisha jamii madhara ya ukeketaji, na kuimarisha juhudi za pamoja ili kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu, na hasa haki za watoto wa kike.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
“Kupitia programu ya Marafiki wa North Mara, tumeweza kuzungumza na wanafunzi zaidi ya 800 kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, na kuhamasisha kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria,” amesema Lyambiko na kuendelea:
“Aidha, kupitia programu hiyo pia tumeweza kuwafikia wanawake 300 kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi ili kuwaeliwesha misingi yetu katika kuheshimu na kulinda haki za binadamu. Ni matumaini yetu kuwa wataendelea kuwa mabalozi wazuri, wakikemea vitendo vya uhalifu, ukatili na uvunjifu wa amani katika jamii.”
GM huyo ameongeza kuwa tafsiri ya mgodi wa North Mara kuhusu haki za binadamu ni pana kwani inagusa uboreshaji huduma na maisha ya jamii, ambapo tangu mwaka 2020 hadi sasa umeweza kuwekeza kwenye miradi 253 yenye thamani ya shilingi bilioni 22 kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Viongozi wa Serikali katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa North Mara.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Viongozi wa Serikali na mgodi wa North Mara katika picha ya pamoja na baadhi ya wazee wa mila waliohudhuria uzinduzi huo.
Viongozi wa Serikali na mgodi wa North Mara na baadhi ya ngariba (wakeketaji) waliohudhuria uzinduzi huo.
Awali, Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jumanne Mkwama amewaomba wazee wa mila kuacha kujihusisha katika hukumu za kesi za ukatili wa kijinsia, badala yake washirikiane na vyombo vya dola kukomesha vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki zabinadamu.

Viongozi wa Serikali na mgodi wa North Mara na baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi waliohudhuria uzinduzi huo.
Katika kampeni hiyo ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, wadau mbalimbali watashirikiana kuendesha midahalo na mikutano ya kuelimisha jamii madhara ya ukatili wa kijinsia, miongoni mwa mada nyingine.
Mbali na Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Tarime na mgodi wa Nora Mara, wadau wengine walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo wakiongozwa na Jeshi la Polisi, ni wazee wa mila, ngariba, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, yakiwemo ATFGM Masanga, HGWT, VSO na timu ya wanasheria kutoka Bowmans.
No comments:
Post a Comment