Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
NA MWANDISHI WETU, Dodoma
SOMO la biashara sasa litakuwa la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia mwakani, Serikali imetangaza.
Nia ya uamuzi huo wa Serikali ni kujenga taifa la Watanzania wenye uwezo wa kufikiri kibiashara na kuondoa hali ya utegemezi wa ajira kutoka sekta ya umma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema.
Kutokana na azima hiyo ya Serikali, Majaliwa ameviagiza vyuo vya biashara kupitia mitaala yao ili kujenga kizazi cha wahitimu wabunifu na walio tayari kufanya biashara badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.
Akifungua kongamano la tano la maendeleo ya biashara na uchumi lililoandaliwa na Chuo cha Biashara Tawi la Dodoma mwishoni mwa wiki, Majaliwa alisema Serikali kwa upande wake kupitia sera ya mafunzo ya mwaka 2023, imeelekeza somo la biashara liwe lazima kwa wanafunzi kuanzia mwakani.
Tanzania kwa sasa ina idadi kubwa ya wahitimu wanaokadiriwa zaidi ya 800,000 wanaomaliza vyuo kila mwaka na kuingia kwenye soko la ajira. Idadi hiyo inailazimisha Serikali kubuni mbinu mbadala za kuzalisha ajira kwenye sekta isiyo rasmi.
No comments:
Post a Comment