NEWS

Saturday, 16 November 2024

Benki Kuu ya Tanzania yawanoa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa kuhusu masuala ya fedha, akiba ya dhahabu na uchumi wa nchi




Na Christopher Gamaina, Mwanza

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewakutanisha waandishi wa habari takriban 40 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, katika semina maalum ya siku mbili ya kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yake, masuala ya fedha, sheria zake na uchumi wa nchi.

Semina hiyo ilifanyika Novemba 14 hadi 15, 2024 jijini Mwanza ambapo BoT iliwaelimisha muundo na majukumu yake, maana ya sera ya fedha inayotumia riba, na utekelezaji wa sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha.

Pia, iliwaelimisha umuhimu wa Benki Kuu kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni, alama za usalama wa fedha na utunzaji wake, na uamuzi wa kuondoa noti za zamani katika mzunguko.


Meneja Msaidizi wa Idara ya Uchumi - BoT, Issa Pagali akiwasilisha mada kuhusu riba za mikopo ya fedha.
------------------------------------------


Meneja Msaidizi wa Kurugenzi ya Masoko ya Fedha - BoT, Dkt Anna Lyimo akiwasilisha mada katika semina hiyo.
------------------------------------------


Afisa Mwandamizi wa Masuala ya Fedha - BoT, Omari Kitojo akiwasilisha mada,
----------------------------------------

Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza linalohudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa, Gloria Mwaikambo alisema lengo kuu la semina hiyo ni kuwawezesha wanahabari hao kutoa habari sahihi na za kuaminika kuhusu shughuli za kifedha na uchumi wa nchi - zinazosimamiwa na benki hiyo.

“Kwa kutambua umuhimu wenu [waandishi wa habari], BoT tumeamua kuwaleta karibu yetu kwa kuwajengea uelewa ili muweze kuwafikishia wananchi taarifa sahihi za uchumi na fedha,” Gloria alisema wakati wa ufunguzi wa semina hiyo.

Alisisitiza kuwa taarifa sahihi za kifedha ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa nchi, hivyo ushirikiano na vyombo vya habari ni muhimu ili kuhakikisha umma unapata habari za kuaminika kuhusu hali ya fedha na uchumi wa taifa.

Mkurugenzi wa BoT Tawi la Landa la Mwanza, Gloria Mwaikambo akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo.
-----------------------------------------

Aidha, waandishi wa habari walielezwa jinsi Benki Kuu inavyoshirikiana na taasisi nyingine kufuatilia na kudhibiti viwango vya riba, usimamizi wa soko la fedha katika kuboresha uchumi wa taifa, changamoto zinazojitokeza na mafanikio ya benki hiyo.

Kwa ujumla, semina hiyo ilionekana kama hatua muhimu katika kuwajemgea waandishi wa habari uwezo wa kuwa mabalozi wazuri wa BoT katika kutoa habari za manufaa kwa umma kuhusu masuala ya fedha na uchumi wa nchi.


Picha ya pamoja
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages