
Na Mwandishi Wetu, Mwanza

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imepata mafanikio makubwa katika unuzuzi wa dhahabu safi, kati ya Julai 2023 na Novemba 2024.
Katika kipindi hicho, benki hiyo imefanikiwa kununua takriban tani moja ya dhahabu safi, rekodi ambayo haikuwahi kufikiwa miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt Anna Lyimo, benki hiyo imeweza kununua kilo 872 za dhahabu safi yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 74 kwa kipindi cha Oktoba mwaka huu (2024) pekee.
“Tukijumlisha na dhahabu [kilo zaidi ya 300] tuliyonunua mwaka jana [2023], hadi sasa hivi tumeweza kununua tani moja ya dhahabu iliyo katika mfumo wa dhahabu fedha,” Dkt Anna alisema.
Alikuwa akizungumza katika semina ya siku mbili iliyoendeshwa na BoT kwa waandishi wa habari takriban 40 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambayo ilihitimishwa Ijumaa iliyopita jijini Mwanza.
Akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa Benki Kuu ya Tanzania kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni, Dkt Lyimo alisema ununuzi wa dhahabu unasaidia kuimarisha akiba hiyo na kuongeza thamani ya fedha nchini, miongoni mwa faida nyingine.
“Faida za ununuzi wa dhahabu ni pamoja na kuimarisha mzigo wa kutosha wa fedha za kigeni, kupandisha thamani ya fedha na kusaidia rasilimali zetu,” aliongeza.
Dkt Lyimo alifafanua kuwa uwekezaji katika dhahabu umekuwa ukitoa faida kubwa kuliko uwekezaji katika njia nyingine mbalimbali kwa miongo miwili iliyopita.

Dkt Anna Lyimo akiwasilisha mada
katika semina hiyo.
---------------------------------------
Kama bidhaa, thamani ya dhahabu inategemeana na upatikanaji, wingi wa dhahabu na jinsi soko la dhahabu linavyotathmini mwenendo wa bei ya dhahabu, alisema Dkt Lyimo.
Aliongeza kuwa akiba ya dhahabu fedha imekuwa ikitumika katika harakati za kuweza kujikimu katika kipindi cha mtikisiko wa kiuchumi duniani.
Mada nyingine zilizowasilishwa na wataalumu kutoka BoT katika semina hiyo, ni muundo na majukumu ya benki hiyo, utekelezaji wa sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha, uamuzi wa kuondoa noti za zamani kwennye mzunguko, alama za usalma wa fedha na utunzaji wake, na sera ya fedha inayotumia tiba.
Awali, akifungua semina hiyo, Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza, Gloria Mwaikambo alisema lengo kuu la semina hiyo ni kuwawezesha wanahabari hao kutoa habari sahihi na za kuaminika kuhusu shughuli za kifedha na uchumi wa nchi - zinazosimamiwa na benki hiyo.
“Kwa kutambua umuhimu wenu [waandishi wa habari], BoT tumeamua kuwaleta karibu yetu kwa kuwajengea uelewa ili muweze kuwafikishia wananchi taarifa sahihi za uchumi na fedha,” alisema Gloria.
Alisisitiza kuwa taarifa sahihi za kifedha ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa nchi, hivyo ushirikiano na vyombo vya habari ni muhimu ili kuhakikisha umma unapata habari za kuaminika kuhusu hali ya fedha na uchumi wa taifa.
Waandishi wa habari walioshiriki semina hiyo, ni kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita na Kagera inayounda Kanda ya Ziwa.
No comments:
Post a Comment