NEWS

Monday, 25 November 2024

Biteko aponda kampeni za matusi



Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dkt Doto Biteko (kulia) akinadi mmoja wa wagombea wa uongozi wa Serikali za Mitaa wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho mkoani Mara uliofanyika katika mji mdogo wa Nyamongo, wilayani Tarime wiki iliyopita. (Picha na Godfrey Marwa)
--------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Tarime

Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Doto Biteko amewahimiza wananchi kuzingatia kuchagua viongozi wa serikali za mitaa wanaotokana na chama hicho tawala akisema ndio watakaongea ‘lugha moja’ naviongozi wa ngazi za juu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya kisekta.

“Chagueni viongozi wanaongea lugha moja na viongozi wa juu. CCM ndiyo italeta maendeleo ya watu,” alisisitiza Dkt Biteko wakati akihutubia mkutano mkubwawa uzinduzi wa kampeni za CCM Mkoa wa Mara uliofanyika kimkoa katika mjimdogo wa Nyamongo, wilayani Tarime wiki iliyopita.

Dkt Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwasihi wananchi kutochukulia poa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuchagua viongozi kwa majaribio.

“Tusifanye majaribio katika kuchagua viongozi. [CCM] tunaomba kura kwa sababu kazi hii tuna uwezo wa kuifanya,” Dkt Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe mkoani Geita alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi kuwakataa wanasiasa na wagombea waliofilisika sera kiasi cha kufanya kampeni za matusi, kuchafua na kuvunjia watu heshima.“Maendeleo hayaletwi kwa matusi, maendeleo hayaletwi kwa kuvunjiana heshima.Msichague mtu wa kuzungumza watu, chagueni mtu wa kuzungumza maendeleo,” alisema.

Aliongeza: “Ninyi [akimaanisha wana-CCM] msijibu mtu kwa tusi, jibuni kwa maendeleo, ushindeni ubaya kwa wema.”

Dkt Biteko alitumia nafasi hiyo pia kugusia utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita akisema maendeleo makubwa ya kisekta yanayoendelea kushuhudiwa nchinichini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ni utekelezaji wa Ilani ya CCM inayoangazia maisha bora kwa wananchi.Rais anataka tupate unafuu wamaisha,” alisema.

Katika uzinduzi huo wa kampeni za CCM, Dkt Biteko aliambatana na viongozi wengine mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi na Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo ambao waliwaomba wananchi kumpaRais Samia zawadi ya kuchagua viongozi wa vijiji na mitaa wanaotokana na chama hicho tawala.

Kampeni za uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa zinatarajiwa kuhitimishwa Novemba 26, kupisha uchaguzi wenyewe uliopangwa kufanyika nchini kote Novemba 27, mwaka huu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages