
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano (kulia) akimkabidhi Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias zawadi ya pakiti zenye kahawa bora duniani inayolimwa Tarime, baada ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na nchi hiyo mkoani Mara wiki iliyopita.
----------------------------------
BALOZI wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias alipoamua kuutembelea mkoa wa Mara hakutarajia kupata mapokezi makubwa na kupewa zawadi lukuki ambazo hakuzifikiria katika maisha yake.
Lakini kwa ukarimu wa wakazi wa Mara, mwanadiplomasia huyo alijikuta ametwishwa mzigo wa kahawa bora duniani na kukabidhiwa kifimbo kama cha Mwalimu Nyerere kutambua mchango wa nchi yake kwa maendeleo ya Tanzania. Tanzania ni nchi ya watu wakarimu, hiyo ndiyo picha aliyoiona Balozi Charlotta mkoani Mara na kubaki katika kumbukumbu zake.
Balozi huyo aliutembelea mkoa wa Mara kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayopata ufadhili wa nchi yake, ambayo imebadili sura ya mkoa wa Mara, hasa katika sekta ya elimu.
Aliishauri Tanzania kufanya mageuzi katika sekta ya elimu kwa kuwa na mtaala mpya ulioboreshwa ili kuhakikisha watoto wanafundishwa kuwa wabunifu, wataalamu na viongozi bora kwa maendeleo ya nchi.
Alisema serikali haina budi kutenga angalau asilimia 20 ya bajeti yake kwa ajili ya elimu na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika katika mambo muhimu yatakayoleta mageuzi na tija kwenye sekta hiyo.
Balozi huyo alitoa ushauri huo alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Alfred Mtambi wiki iliyopita alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Global Partnership for Education (GPE) Lanes II.
“Nimefurahi sana kushiriki katika kuitembelea miradi inayofadhiliwa na nchi yangu na Global Partnership for Education (GPE) ambayo ni muunganiko wa nchi 90 duniani zinazochangia miradi mbalimbali ya elimu yenye lengo la kuboresha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13,” alisema Balozi Charlotta.
Alisema ziara hiyo ya siku nne katika mikoa ya Arusha na Mara, ni sehemu ya ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na washirika wa GPE Lanes II kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
Aliipongeza Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo kwani imeleta matokeo chanya. “Lengo la mradi linaweza kutimizwa kama kutakuwa na mgawanyo wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na kuhakikisha walimu wenye sifa wameajiriwa katika shule zote zenye mahitaji,” alisema.
Akizungumza baada ya mapokezi ya Balozi Charlotta na msafara wake, Kanali Mtambi alisema mkoa wa Mara umesimamia vizuri miradi yote iliyopokea fedha kutoka mradi wa GPE Lanes II na kumhakikishia kwamba fedha zote zitakazoletwa baadaye zitatumika vizuri.
.jpg)
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Alfred Mtambi (kulia) akimkabidhi Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias zawadi ya kirungu alipomtembelea ofisini kwake mjini Musoma wiki iliyopita.
------------------------------------
“Miradi yote tuliyoitekeleza kutokana na mradi huu imetekelezwa vizuri na mkiitembelea mtaweza kuona mambo makubwa yaliyofanyika kutokana na fedha tulizopokea. Niwahakikishie tukipewa fedha zaidi tutazitumia vizuri,” alisema.
Mtambi alisema ufadhili wa miradi hiyo unatokana na sera nzuri za kimataifa za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uhusiano na nchi nyingine.
Aliishukuru Sweden kwa ufadhili huo na kwa kuimarisha sekta ya elimu katika mkoa wa Mara, na akaiomba nchi hiyo iendelee kuusaidia pia katika sekta ya afya na uwezeshaji wa vijana katika sekta za madini na uvuvi, ili kukuza uchumi endelevu wa wananchi wa Mara.
Maeneo mengine ambayo Kanali Mtambi alisema yanahitaji msaada ni mapambano dhidi ya mila ya ukeketaji wasichana, tatizo ambalo linaharibu maisha na kuua ndoto zao.
Aidha, Kanali Mtambi alitumia fursa ya kukutana na Balozi Charlotta kuomba GPE Lanes II kuja kuwekeza mkoani Mara, hasa katika sekta za uchimbaji wa madini, utalii, kilimo na maeneo mengine watakayoona yanafaa.
No comments:
Post a Comment