
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan (katikati) akiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) alipokwenda kujionea ghorofa lililoporomoka eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam jana.
----------------------------------------
Watu 20 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa katika tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, taarifa iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan imeeleza.
Janga hilo lilitokea Jumamosi iliyopita Novemba 16, 2024 majira ya asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa aliyokabidhiwa Rais baada ya kurejea nchini jana kutoka Rio de Janeiro, Brazil, kuanguka kwa jengo hilo ni matokeo ya kutowajibika kwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa masuala ya ujenzi.
Ukweli halisi wa tukio la kuanguka kwa jengo hilo utabainika baada ya tume iliyoundwa kuchunguza tukio hilo na ukaguzi wa majengo yote ya Kariakoo kukamilisha kazi hiyo.
Tume hiyo inaongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Rais Samia ambaye alikuwa Brazil kuhudhuria mkutano wa mataifa tajiri (G 20), jana alikwenda moja kwa moja kwenye eneo la ajali hiyo baada ya kuwasili Dar es Salaam.
Aliwambia wananchi waliokusanyanyika kwenye ghorofa ililoporomoka kwamba jitihada za serikali ziliekekezwa zaidi katika kuwaokoa watu waliofukiwa na kifusi cha jengo hilo.
Rais Samia ambaye baadaye alielekea Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwajulia hali majeruhi, alisema janga la kuanguka kwa jengo hilo siyo tu ni pigo kwa familia za marehemu na majeruhi, bali pia ni pigo kwa taifa.
Aliwashukuru watu wote na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kujitoa mhanga katika shughuli za uokoaji.
Kiongozi huyo wa nchi aliahidi kuwaalika Ikulu ili kuwapa shukrani maalum waokoaji wote walioshiriki katika tukio hilo.
No comments:
Post a Comment