NEWS

Wednesday, 27 November 2024

RC Mtambi awapongeza wana-Mara akipiga kura mtaani kwake



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi akipiga kura kuchagua viongozi wa mtaa wake mjini Musoma leo.

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa katika kituo kilichopo Ofisi ya Kata ya Mukendo, Manispaa ya Musoma na kuwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa ukomavu wa kisiasa, na kuwataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Mtambi amesema katika kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wananchi walionesha ukomavu wa kisiasa ulioziwezesha kufanyika kwa amani na utulivu, bila kuwepo malalamiko ya vyama, au wagombea kufanyiwa fujo.

“Ninawapongeza wananchi wa mkoa wa Mara kwa ukomavu mkubwa wa kisiasa waliouonesha katika kipindi chote cha kampeni na ninawakumbusha kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka,” amesema.

Aidha, Kanali Mtambi amevitaka vyama vya siasa na wanachama wao kuheshimu na kuzifuata kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo walishiriki kuzitunga na kama kuna malalamiko yoyote wanaweza kuyawasilisha sehemu zinazohusika kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi.

Ametumia nafasi hiyo pia kupiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima wakati huu wa uchaguzi na kuwataka wananchi kuhakikisha kuwa baada ya kupiga kura wanaenda kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Kiongozi huyo wa mkoa pia amewaonya watu wanaopanga kufanya vurugu akitahadharisha kuwa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara na wananchi hawatamvumilia mtu yoyote atakayeanzisha fujo katika kipindi hiki, kwani Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akizungumza katika eneo hilo naye amewaomba wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi na kuwahakikishia usalama wao wakati wote.

Chikoka pia amewataka wananchi kuachana na mikusanyiko isiyo ya lazima na kutoa taarifa kwa viongozi wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa 2:00 asubuhi na vinatatajiwa kufungwa saa 10:00 jioni, na baada ya kupiga kura wananchi wanashauriwa kuondoka katika eneo la kituo cha kupiga kura kwa utulivu na amani.

Leo Novemba 27, 2024 ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo wananchi wanachagua viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa mitaa/ vijiji, wajumbe wa serikali ya mtaa/ kijijji, wenyeviti wa vitongoji.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya uchaguzi huo inasema: “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages