NEWS

Tuesday, 17 December 2024

Mama Samia Legal Aid yafikisha msaada wa kisheria bila malipo kwa wananchi mkoani Mara




Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea katika mkoa wa Mara kwa kufikisha huduma za msaada wa kisheria bila malipo kwa wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi vijijini.

“Kampeni hii imeanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili kupunguza migogoro, kudumisha amani, kuleta maendeleo na kuimarisha misingi ya upatikanaji haki nchini.

“Pia, kupokea na kutatua changamoto za kimaendeleo kwa wananchi,” Msajili Msaidizi wa watoa huduma za msaada wa kisheria katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mussa Maulid Magope ameiambia Mara Online News kwa simu leo Desemba 17, 2024.

Mussa ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, amesema kampeni hiyo kwa mkoa wa Mara ilizinduliwa Desemba 11, 2024 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ili kuzifikia halmashauri zote tisa za mkoa huo.

“Kampeni hii imelenga kuzifikia kata 10 kwa kila halmashauri na vijiji vitatu kwa kila kata,” Mussa amefafanua.

Amebainisha kuwa kata zilizolengwa na kampeni hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni Muriba, Matongo, Nyamwaga, Sirari, Nyakonga, Gorong'a, Kibasuka, Komaswa, Susuni na Mwema.


Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanapatiwa elimu ya sheria mbalimbali, nafasi ya kuwasilisha changamoto zao na kupata msaada wa kisheria kwa mtu mmoja mmoja.

Kampeni hiyo, yenye kaulimbiu inayosema “Huduma za Msaada wa Kisheria kwa Haki, Amani na Maendeleo”, itahitimishwa Desemba 20, 2024 katika kata za Susuni na Mwema.

“Baada ya hapo madawati ya msaada wa kisheria yaliyopo ofisi za Mkurugenzi Mtendaji yataendelea kutoa huduma hizo kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii,” amesema Mussa na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma za msaada wa kisheria ambazo Rais Samia amekusudia ziwafikie wananchi wote nchini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages