
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo akionesha Tuzo aliyotunukiwa.
-------------------------------
Baraza la Jumuiya ya CCM ya Wazazi Wilaya ya Musoma Vijijini limemtunuku Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, Tuzo ya pongezi na kutambua ushiriki na mchango wake mkubwa wa fedha kwenye uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.
Prof Muhongo alipongezwa na kukabidhiwa Tuzo hiyo kwenye kikao cha Baraza hilo kilichofanyika kijijini Murangi, jimboni humo jana Desemba 17, 2024, mgeni rasmi akiwa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Mara, Simon Rubugu.
Kikao hicho pia kilitathmini masuala mbalimbali kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika jimbo hilo, ambapo chama tawala - CCM kilipata ushindi wa kishindo.
Pia, wajumbe walielezwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, lakini pia mafanikio yanayopatikana Musoma Vijijini kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.
Vilevile, washiriki wa kikao hicho walielezwa vipaumbele vya sasa na vya miaka ijayo vya mahitaji ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini.
Aidha, viongozi wa CCM na jumuiya zake za Wazazi, UWT na UVCCM ngazi za wilaya, kata na matawi walipongezwa kwa kujituma ipasavyo hadi kukiwezesha chama hicho kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa.
Katika uchaguzi huo, CCM kilishinda katika vijiji 66 sawa na asilimia 97.06 na vitongoji 358 (asilimia 95.72), huku CHADEMA kikiambulia vijiji viwili na vitongoji 16.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Basi la Kisire lapata ajali Magu, baadhi ya abiria wahofiwa kufa
>>Vinicius Jr ashinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa FIFA
>>Dkt Machage atembelea ofisi za Gazeti la Sauti ya Mara, alipongeza kwa kazi nzuri
>>TAMISEMI yatangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2025
No comments:
Post a Comment