
Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha.
Na Mwandishi Maalumu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imewapa wateja wake waliokatiwa maji ofa ya kipekee ya kuwarejeshea huduma hiyo bila sharti la kulipa faini katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa tangazo kwa umma lililotolewa na MUWASA, ofa hiyo ilianza Desemba 20, 2024 na itaendelea hadi Januari 20, 2025.
Ilifafanua kuwa mteja aliyekatiwa maji kutokana na kushindwa kulipa bili kwa wakati, atarudishiwa huduma na kupewa mkataba wa kulipa deni lake kidogo kidogo ili kujidumishia huduma hiyo.
MUWASA imezingatia kuwa wakati wa sikukuu mahitaji ya maji huwa makubwa, hivyo ofa hiyo itawezesha wateja wa mamlaka hiyo kufurahia sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya bila kikwazo cha maji.
Pia, mamlaka hiyo inaamini kuwa hatua hiyo itawawezesha wateja wengi kurudi katika mtandao wake na kufurahia huduma muhimu ya majisafi na salama ya bomba kipindi hiki cha sikukuu na kuendelea.
MUWASA inaendelea kutekeleza mipango mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuboresha huduma ya majisafi na salama ya bomba katika miji ya Musoma, Mugumu, Tarime na Shirati, mkoani Mara.
Kwa upande wa Musoma, tayari MUWASA imeshafikia lengo la Ilani ya CCM ya kufikia asilimia 95 ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi mijini kufikia 2025.
No comments:
Post a Comment