NEWS

Monday, 23 December 2024

Tarime: Benki ya CRDB yafungua tawi Sirari


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati waliokaa) na viongozi wa CRDB, miongoni mwa wengine wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha ngoma ya asili wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo Sirari leo Desemba 23, 2024.
------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Benki ya CRDB imezindua rasmi tawi lake jipya katika mji mdogo wa Sirari, mkoani Mara mpakani na Kenya.

Uzinduzi wa tawi hilo umefanyika leo Desemba 23, 2024 na kushuhudiwa na viongozi wa wilaya ya Tarime, wananchi na wafanyakazi wa benki hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Benki ya CRDB Tawi la Sirari leo Desemba 23, 2024.
-------------------------------------

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele ametoa wito wa kuhamasisha wakazi wa Sirari na maeneo jirani kuchangamkia huduma zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara.

Meja Gowele amesema uwepo wa benki hiyo utaongeza usalama wa fedha za wananchi katika eneo hilo, miongoni mwa faida nyingine.


Picha ya pamoja mbele ya Benki ya CRDB Tawi la Sirari
--------------------------------

Uzinduzi wa tawi la Sirari linafanya idadi ya matawi ya benki hiyo kufikia 10 katika mkoa wa Mara kwa sasa, huku wilaya ya Tarime ikiongoza kwa kuwa na matawi mengi.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Benki ya CRDB Tawi la Sirari.
----------------------------------

Meja Gowele ametumia nafasi hiyo pia kuiomba Benki ya CRDB kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za kibenki.

“Muwape wananchi elimu juu ya umuhimu wa kuweka akiba lakini pia umuhimu wa kukopa na kurejesha kwa wakati, na kufanya malipo kupitia benki,” amesisitiza kiongozi huyo wa wilaya.

Ameongeza: "Nitoe rai kwenu watu wa CRDB pia kuweka masharti na vigezo nafuu, ikiwemo kutoa riba nafuu ili wananchi kunufaika na huduma mnazotoa na kuachana na mikopo ya mitaani yenye riba kubwa."

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Boma Raballa amewataka wafanyabiashara wa mkoani Mara kuchangamkia fursa za uwekezaji katika benki hiyo, ikiwa ni pamoja na kununua hatifungani zinazojulikana kama 'Samia Infrastructure Bond'.

"Nitumie fursa hii kuwahamasisha wawekezaji hapa Sirari, Tarime na mkoa mzima wa Mara kuchangamkia fursa hii [hatifungani za Samia Infrastructure Bond] kwa kuwa inatoa faida nzuri," amesema Raballa.

Katika hatua nyingine, Benki ya CRDB imetumia hafla hiyo kukabidhi msaada wa madawati 50 kwa DC Gowele ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha mazingira ya elimu katika wilaya hiyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages