NEWS

Sunday, 29 December 2024

Maswi akerwa chuki za kisiasa kukwamisha maendeleo ya wananchi Tarime Vijijini



Eliakim Chacha Maswi

Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Chacha Maswi ameeleza kukerwa na chuki za kisiasa kutumika kukwamisha maendeleo ya wananchi katika jimbo la Tarime Vijijini.

Maswi ‘alitema nyongo’ hiyo katika hafla ya kukabidhi gari la kubeba wagongwa kwa Kituo cha Afya Magoto juzi, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara.

Maswi ambaye hata hivyo hakutaja jina la mtu, alikemea vikali migawanyiko ya kisiasa inayodhoofisha ushirikiano wa jamii na kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alifafanua kuwa chuki za kisiasa zimekuwa kikwazo katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya huduma za kijamii katika jimbo hilo, akitolea mfano Kituo cha Afya Magoto na barabara ya kuingia kijijini hapo.

“Barabara ni mbovu imeshindwa kupitika... Niliomba shilingi milioni 378 ili kupanua Kituo cha Afya Magoto lakini fedha hazikufika kwa sababu mbunge alipiga simu zisitoke,” alisema Maswi.

Alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kutafuta njia za kumaliza migogoro na kuchochea maendeleo badala ya kuongeza migawanyiko.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi wa jimbo hilo na kuachana na siasa za chuki zinazozorotesha juhudi za kuleta maendeleo.

Maswi alihitimisha kwa kutoa wito wa mshikamano wa viongozi na siasa za udugu zinazojali maslahi na maendeleo ya jamii nzima.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Mbunge Waitara ili kujua kauli yake kuhusu tuhuma za kuzuia fedha zilizoombwa na Maswi kwa ajili ya uboreshaji wa Kituo cha Afya Magoto.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages