
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ameteua na kubadilisha viongozi mbalimbali, wakiwemo Mawaziri, Mabalozi na Makatibu wa Wizara.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Desemba 9, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt Moses Kusiluka, Rais Samia amehamisha majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwennda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Ambapo Prof Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Aidha, Rais Samia amemteua Jerry William Silaa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na Dkt Damas Daniel Ndumbaro kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wakati Dkt Ashatu Kachwamba Kijaji ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mawaziri wengine walioteuliwa na wizara zao zikiwa kwenye mabano ni Abdallah Hamis Ulega (Ujenzi) na Innocent Lugha Bashungwa (Mambo ya Ndani ya Nchi).
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Kwa upande mwingine, James Henry Kilabuko ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), huku Dkt Stephen Justice Nindi akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji).
Dkt Suleiman Hassan Serera yeye amehamishwa kutoka Wizara ya Kilimo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, wakati Balozi Dkt John Stephen Simbachawene atapangiwa kituo cha kazi.
Kwa upande wake Prof Mohamed Yakub Janabi ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Tiba huku akiendelea kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wengine ni Anderson Gukwi Mutalembwa, Mobhare Matinyi, aliyekuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Hamad Khamis Hamad, CP Suzan Kaganda na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba - ambao wameteuliwa kuwa Mabalozi wanaosubiri kupangiwa vituo vya kazi.
“Uapisho wa viongozi mbalimbali walioteuliwa utafanyika Ikulu Ndogo, Tanguu Zanzibar tarehe 10 Desemba 2024 kuanzia saa 5:00 asubuhi,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>HABARI PICHA:Waandishi wa habari Mara kushiriki kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
>>Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kufanya ziara ya siku nne mkoani Mara
>>Rais wa Syria adaiwa kuikimbia nchi, waasi wafungulia wafungwa gerezani
>>Wabunge wa Tanzania wapata ajali wakienda mashindano ya michezo Kenya
No comments:
Post a Comment