
Paul Thomas Mwikwabe
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa anayewakilisha Mkoa wa Mara, Paul Thomas Mwikwabe, anatarajia kufanya ziara ya siku nne ya kuhamasisha uhai wa jumuiya hiyo katika wilaya zote za mkoa huo.
Paul ameiambia Mara Online News kwa simu leo kwamba amepanga kufanya ziara hiyo kuanzia Desemba 10 hadi 13, 2024, ambapo ataanzia Musoma Vijijini, kisha kuendelea Bunda, Musoma Mjini, Butiama, Rorya, Tarime na kuhitimisha wilayani Serengeti kwa kuhutubia mkutano wa hadhara.
Amesema atatumia fursa hiyo kukutana na kuzungumza na vikundi vya vijana vinavyonufaika na mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri za miji na wilaya zao, kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025, na vilevile, atakutana na kuzungumza na waendesha 'bodaboda' na mama lishe katika wilaya hizo.
Pia, atawapongeza na kuwashukuru vijana kwa kushiriki na kukipatia chama tawala - CCM ushindi mkubwa katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchini kote Novemba 27, 2024.
“Nitatumia ziara hiyo pia kuhamasisha vijana kuhusu umuhimu wa kujipanga kisiasa kwa ajili ya katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Mwaka 2025,” ameongeza Paul.
Aidha, katika mikutano yake, Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa atasisitiza umuhimu wa vijana kuweka mipango mikakati ya kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushinda katika chaguzi na kuchochea maendeleo ya mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.
Kimsingi, ziara hiyo inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya kukiimarisha chama hicho tawala na kuhamasisha ushirikiano wa pamoja kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment