NEWS

Friday, 3 January 2025

Asanteni sana wasomaji wetu wa Mara Online News, Sauti ya Mara



Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Mhariri Mtendaji (ME) wa Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, Mugini Jacob Mwera.
--------------------------------------------

Kwanza kabisa, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuuona mwaka mpya 2025. Mwaka uliopita [2024], kama ilivyo miaka mingine iliyotangulia, ulikuwa ni mwaka uliojaa mambo mengi ya kufurahisha na kuhuzunisha. Furaha na kilio ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.

Sisi SAUTI YA MARA na MARA ONLINE NEWS, tunawashukuru sana wasomaji wetu wa kila tabaka katika jamii yetu. Kwa hakika, katika mwaka uliopita mmetutia moyo katika kufanya kazi hii ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma.

Kazi hii ya kukusanya, kuandaa na kusambaza habari ni ngumu katika dunia hii ya dijiitali iliyojaa ushindani wa kila aina. Lakini tunashukuru kwamba kupitia wasomaji wetu, kazi hii imeonekana kuwa nyepesi kutokana na mrejesho tunaopata wa kututia moyo.

Wapo wasomaji wetu waliotukosoa kwa nia njema kabisa; hao tunawambia asanteni sana na tutafuata ushauri wenu mzuri. Wapo wasomaji wetu waliotumwagia sifa; nao tunawambia asanteni sana.

Sisi tunachokitaka kutoka kwa wasomaji wetu ni kuambiwa ukweli, ukweli na ukweli mtupu bila ya fitina ndani yake. Kwa hakika, tunawashukuru waliotusifu na wale waliotukosoa; wote wamefanya jambo jema katika kuendeleza fani hii ya uandishi wa habari.

Matarajio ya 2025
Tunaahidi kwamba mwaka mpya wa 2025 tutawaletea habari motomoto kwa kila sekta ya maendeleo kuanzia ngazi ya kaya, kitongoji, kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa.

Lengo letu ni kuhakikisha kwamba Gazeti la SAUTI YA MARA na MARA ONLINE NEWS, vinakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya mkoa wa Mara na taifa letu kwa ujumla.

Mkoa wetu wa Mara umejaaliwa kila aina ya raslimali kama vile madini, wanyamapori, mifugo, samaki katika Ziwa Victoria na Mto Mara na ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao ya aina zote. Lakini pia, mkoa huu unatambulika duniani kwa kuzalisha kahawa bora aina ya Arabica inayolimwa wilayani Tarime.

Kivutio cha uwekezaji
Rasilimali hizi zote zilizotajwa hapo juu ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania. Sisi wa SAUTI YA MARA na MARA ONLINE NEWS tunaahidi kwamba tutafanya kila linalowezekana kutangaza fursa hizi za uwekezaji ili mkoa wetu uwe sumaku ya kuwavuta wawekezaji katika kila sekta ya maendeleo.

Tunawaomba viongozi na wadau wote wa maendeleo kutupa ushirikiano wa kutosha ili kurahisisha harakati zetu za ukusanyaji na usambazaji wa habari.

Hakuna ubishi kwamba mkoa wetu wa Mara ni chimbo maarufu la habari kwa Tanzania kwa sababu kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazofanyika bila kutangazwa. Kinachotakiwa ni ushirikiano wa kufichua shughuli hizi ili zijulikane kwa wananchi wengi. Habari ni nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo, ni kurunzi, nyota na mbalamwezi inayomulika kwenye giza.

Kwa hakika, tunawashukuru viongozi wa ngazi mbalimbali wa taasisi za umma na binafsi mkoani Mara kwa kutupa ushirikiano wa hali ya juu katika jukumu letu mama la kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma.

Tunaahidi kuendelea 'kuwalisha' wasomaji wetu wa MARA ONLINE NEWS na SAUTI YA MARA habari na makala za maendeleo ya kisekta - zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina na kwa weledi mkubwa, kwa manufaa ya jamii nzima.

Mungu wabariki wasomaji wetu, ubariki mkoa wa Mara, ibariki Tanzania, ibariki Afrika. Amina.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages