NEWS

Thursday, 2 January 2025

Vijiji vinavyofaidi mrabaha kutoka Mgodi wa Barrick North Mara vinapaswa kuwa ‘Paradiso’ Tarime Vijijini



Lori likiwa kazini katika Mgodi
wa Dhahabu wa North Mara.

Na Christopher Gamaina
chris_pressman@yahoo.com

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) ni chanzo kikuu cha mapato ya fedha za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji vinavyouzunguka, hasa vile vinavyopata gawio la mrabaha.

Vijiji vinavyopata gawio la mrabaha kutoka mgodi huu ni Nyangoto, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Kewanja ambavyo ni miongoni mwa vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huu.

Vijiji hivi vitano vilikuwa na haki ya kuchimba dhahabu kwenye shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya mgodi wa North Mara) kabla ya Kampuni ya Barrick kukabidhiwa uendeshaji wa mgodi huu kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.

Ikumbukwe kwamba baada ya Barrick kuchukua dhamana ya uendeshaji wa mgodi huu, ilifanya tafiti za kijiolojia katika shimo la Nyabigena na kufanikiwa kuanza tena uzalishaji wa dhahabu katika robo ya pili ya mwaka 2023, baada ya kuwa umesimama tangu mwaka 2017.

Kurejea kwa uzalishaji katika shimo hilo kumevipatia vijiji hivi vitano matumaini mapya ya kuendelea kupata gawio la mrabaha kama ilivyokuwa awali. Malipo ya mrabaha hufanyika kila robo ya mwaka kutokana na hali ya uzalishaji na uuzaji wa dhahabu.

Mfano, Desemba 9, 2024, vijiji hivi vilipata gawio la mrabaha la shilingi bilioni 2.1, ikiwa ni malipo ya robo ya tatu ya mwaka 2024, ambapo Genkuru kilipata shilingi 746,461,112, Nyangoto (shilingi 581,176,695), Kerende, (shilingi 454,221,570), Nyamwaga (shilingi 225,997,310) na Kewanja (shilingi 98,350,773).

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, malipo haya ya shilingi bilioni 2.1 yanafanya gawio la mirabaha lililotolewa na mgodi huo kwenda katika vijiji hivi - kutokana na uzalishaji wa Aprili 2023 hadi Septemba 2024 kufikia shilingi bilioni 4.471.


Wenyeviti wa vijiji wakionesha mifano ya hundi za malipo ya gawio la mrabaha la shilingi bilioni 2.1 yaliyotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Norh Mara, mbele ya Waziri Dkt Dorothy Gwajima (wa tatu kushoto waliokaa) katika hafla iliyofanyika Desemba 9, 2024 Nyamongo, wilayani Tarime.
--------------------------------------

Mfumo huu wa kupata malipo ya mrabaha kila robo ya mwaka unavipa vijiji hivi uhakika wa mapato ya fedha kwa ajili ya kujenga na kuboresha miradi ya kijamii na kiuchumi kwa ustawi na maendeleo ya wananchi.

Kwa hiyo, gawio la mrabaha ni fursa kubwa ya maendeleo katika vijiji hivi vitano. Iwapo fedha hizo zitasimamiwa na kutumika vizuri zinaweza kuvifanya vijiji hivi kuwa ‘Paradisho’ ya maendeleo ya kisekta Tarime Vijijini.

Mirabaha inayotolewa inadhihirisha kwamba mgodi huu wa Barrick North Mara si tu ni chanzo kikuu cha mapato, bali pia ni mtaji muhimu katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijiji hivi vitano, tofauti na vijiji vingine vya Tarime Vijijini vipatavyo 83 ambavyo havina fursa hii.

Kupitia fedha za mirabaha inayotolewa na mgodi huu, vijiji hivi vinaweza kuboresha huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara, huku pia zikitumika kugharimia uanzishaji wa miradi ya kiuchumi kwa ajili ya mapato endelevu, sambamba na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana.

Miradi ya kimkakati ya kiuchumi inaweza kuwa kilimo, biashara, masoko ya kisasa na vivutio vya utalii ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa ustawi wa jamii katika vijiji hivi.

Miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa katika kuboresha huduma za kijamii na maisha ya wananchi na kuongeza fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande mwingine, uboreshaji wa miundombinu ya barabara utaongeza urahisi wa watu kufikia masoko, vituo vya afya, shule na huduma nyingine muhimu za kijamii, na hivyo kupunguza vikwazo kama ambavyo vinawakabili wananchi wa vijiji vingine ambavyo havipati gawio la mrabaha.

Mbali na fedha za mrabaha, vijiji hivi vitano pia vinaendelea kunufaika na mabilioni ya fedha za mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR) kutoka mgodi wa Barrick North Mara. Fedha hizo zinazotolewa na Barrick kwa lengo la kusaidia na kuimarisha ustawi wa wananchi katika maeneo yanayozunguka mgodi huo, ambapo kwa sasa zimekuwa zikigharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali katika vijiji vyote 88 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Kutokana na fursa hizi za mapato, vijiji hivi (Nyangoto, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Kewanja) vinapaswa kuwa Paradiso ya maendeleo ya kisekta kama vile huduma za kijamii zilizoboreshwa, fursa nyingi za ajira na biashara kwa ajili ya ustawi wa wananchi.

Kwa kuzingatia mchango mkubwa wa fedha hizi, vijiji hivi vitano vinapaswa kuonesha utofauti mkubwa, mfano wa maendeleo na ustawi wa wananchi, tofauti na vingine ambavyo havina fursa ya kupata gawio la mrabaha.

Fedha za mirabaha zinazotolewa na mgodi wa Barrick North Mara kwenda kwenye vijiji hivi ni nyingi, zinatosha kuvifanya kuwa Paradiso ya maendeleo Tarime Vijijini kwa kupaisha maendeleo ya kisekta na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa hakika, vijiji vya Nyangoto, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Kewanja vina kila sababu ya kuwa Paradiso ya maendeleo ya kisekta Tarime Vijijini ambapo wananchi wanafurahia maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayotokana na fedha za mirabaha. Inawezekana.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages