NEWS

Thursday, 23 January 2025

Barrick yatumia dola milioni 573 kwa wasambazaji, watoaji huduma wazawa



Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow (kushoto) akizungumza katika mkutano na wadau kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu jana. Kulia ni Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Kahama

Kampuni ya Barrick imetumia dola za Kimarekani milioni 573 (sawa na shilingi za Kitanzania zaidi ya trilioni moja) kwa ajili ya wasambazaji na watoa huduma wa ndani (wazawa) nchini Tanzania, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 83 ya matumizi yote ya kampuni hiyo kwa mwaka jana.

“Aidha, asilimia 75 ya malipo yetu yote kwa watoa huduma na wasambazaji yalikwenda kwa kampuni za wazawa, yakivuka lengo letu la asilimia 61,” Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Dkt Mark Bristow alisema jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Dkt Bristow alikuwa akitoa taarifa kuhusu jinsi ubia wa Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals ulivyochochea utengenezaji enedelevu wa thamani katika uchumi wa Tanzania.

Aidha, kutokana na sera ya Barrick ya kutoa ajira na maendeleo ya ndani, alisema asilimia 96 ya wafanyakazi wake wapatao 6,186 ni Watanzania, huku asilimia 53 wakitoka jamii zinazozunguka migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na North Mara uliopo wilayani Tarime, mkoani Mara.

Pia mwaka jana, Barrick iliwekeza dola zaidi ya milioni tano (shilingi zaidi ya bilioni 12) katika miradi ya maji safi ya kunywa, huduma za afya na elimu, na kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi ya kijamii kufikia dola milioni 15.8 (shilingi bilioni 39.5) tangu ichukue jukumu la uendeshaji wa migodi hiyo mwaka 2019.

Baadaye akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Tanzania, Dkt Steven Kiruswa aliupongeza Barrick kwa jududi kubwa inazofanya kugusa maisha ya wananchi kupitia miradi ya kijamii, kiuchumi na ajira, ambapo alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wawekezaji wengine nchini kuiga mfano huo.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa akizungumza katika mkutano huo.
------------------------------------

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na viongozi wa serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, miongoni mwa wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages