NEWS

Saturday, 25 January 2025

Rais wa Barrick akabidhi msaada wa shilingi milioni 100 kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu



Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow (kulia) akimkabidhi Meneja Miradi wa Shirika la ATFGM Masanga, Valerian Mgani (aliyevaa fulana), mfano wa hundi ya shilingi milioni 25 katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga juzi.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Kahama

Shirika lisilo la kiserikali na vikundi vitatu kutoka maeneo tofauti nchini Tanzania vimepokea msaada wa shilingi za Kitanzania milioni 100 (sawa na dola za Kimarekani 40,000) kutoka Taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP) iliyoanzishwa na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni Barrick, Dkt Mark Bristow.

Shirika ATFGM Masanga, Bulyanhulu Agriculture Group, Fageme Women Group na Youth Wellbeing Initiative, kila kimoja kimepewa shilingi milioni 25.

Dkt Bristow alikabidhi mfano wa hundi za fedha hizo kwa viongozi wa vikundi hivyo juzi katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliyopo wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Viongozi wa vikundi hivyo walishukuru kupata msaada huo na kuahidi kwenda kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Taasisi ya NVeP inasaidia mashirika na vikundi nchini Tanzania, ambapo kila kimoja kilichokidhi vigezo hupewa dola 10,000 kwa ajili ya kusaidia makundi ya wanawake na watoto wenye mahitaji maalumu.

Awali, Dkt Bristow aliwasilisha kwa waandishi wa habari taarifa kuhusu jinsi ubia wa Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni tanzu ya Twiga Minerals ulivyochochea utengenezaji enedelevu wa thamani katika uchumi wa Tanzania.

Alisema Barrick imetumia dola za Kimarekani milioni 573 (sawa na shilingi za Kitanzania zaidi ya trilioni moja) kwa ajili ya wasambazaji na watoa huduma wa ndani (wazawa) nchini Tanzania, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 83 ya matumizi yote ya kampuni hiyo kwa mwaka jana.


Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow (kushoto) akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido.
-----------------------------------------

“Aidha, asilimia 75 ya malipo yetu yote kwa watoa huduma na wasambazaji yalikwenda kwa kampuni za wazawa, yakivuka lengo letu la asilimia 61,” alisema Dkt Bristow.

Kwa upande mwingine, alisema asilimia 96 ya wafanyakazi 6,186 wa Barrick nchini Tanzania ni wazawa, huku asilimia 53 wakitoka jamii zinazozunguka migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na North Mara uliopo wilayani Tarime, mkoani Mara.

Pia mwaka jana, Barrick iliwekeza dola zaidi ya milioni tano (shilingi zaidi ya bilioni 12) katika miradi ya maji safi ya kunywa, huduma za afya na elimu, na kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi ya kijamii kufikia dola milioni 15.8 (shilingi bilioni 39.5) tangu ichukue jukumu la uendeshaji wa migodi hiyo mwaka 2019.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, miongoni mwa viongozi wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages