
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda akikabidhi tuzo kwa Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Barrick Tanzania, Georgia Mutagahywa wakati wa hafla ya tuzo za mlipa kodi bora iliyofanyika Dar es Salaam wiki hii.
--------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara umetwaa tuzo ya uzingatiaji wa kanuni za kodi kitaifa na kwenye sekta ya madini katika kipindi cha mwaka 2023-2024.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa walipa kodi iliandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam wiki hii.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa The Dome, Dar es Salaam, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia aliipongeza TRA kwa ukusanyaji wa kodi, kupanua wigo wa kodi na kuwekeza katika teknolojia muhimu iliyochochea ufanisi kutokana na uwezo wake wa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali.
Migodi ya Dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu uliopo wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga inaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni tanzu ya Twiga Minerals tangu mwaka 2019.
Mwaka 2024, Twiga Minerals ililipa kodi ya mapato kiasi cha dola za Kimarekani milioni 92, mwaka 2023, dola milioni 58 na mwaka 2022 dola milioni 112.
Akiwa katika mgodi wa Bulyanhulu wiki iliyopita, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Dkt Mark Bristow alisema Twiga Minerals imechangia katika uchumi wa Tanzania dola za Kimarekani bilioni 4.24 tangu ilipoanzishwa mwaka 2019. Kati ya hizo, dola bilioni 1.37 zililipwa kwa njia ya kodi na tozo mbalimbali za serikali.
Kwa upande wa uwezeshaji biashara, Dkt Bristow alisema asilimia 83 ya manunuzi ya kampuni kwa mwaka 2024 ambayo ni dola milioni 573 yalifanyika hapa nchini. Kampuni hiyo imetumia dola bilioni 2.3 kwa manunuzi ya ndani tangu 2019.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Viongozi wa Afrika wakutana Tanzania kujadili kuhusu nishati
>>Serengeti na Ngorongoro: Serikali ya Ujerumani, TANAPA, FZS wazindua miradi ya kijamii iliyogharimu mamilioni ya fedha
>>NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha nne 2024
>>Dodoma: Stephen Wasira achaguliwa kwa kishindo kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara
No comments:
Post a Comment