
Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Humphrey Kaaya (wa tatu kulia) akikabidhi sehemu ya msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya shule za msingi Salama A na Salama B wilayani Bunda jana.
----------------------------------
Benki ya NMB imezipatia shule za msingi Salama A na Salama B za wilayani Bunda, Mara msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 10.
Msaada huo wa mabati, mbao na misumari uliombwa na shule hizo baada ya vyumba vitatu vya madrasa kuezuliwa na upepo mkali uliombatana na mvua Agosti 2024.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo jana, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Humphrey Kaaya alisema wametoa msaada huo kwa ajili ya kuezeka vyumba hivyo ili wanafunzi warejee kuvitumia.
Kaaya alisema suala la elimu ni moja ya vipaumbele vya Benki ya NMB kwani ndiyo silaha muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Humphrey Kaaya misumari kwa Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda (Vijijini), Mwalimu Deusdedith Bimbalilwa.
----------------------------------------
“Sisi NMB changamoto ya sekta ya elimu ni jambo la kipaumbele kwani elimu ni ufunguo wa maisha na kiungo kikuu cha maendeleo ya jamii na nchi. Tunaamini bila elimu bora hata sisi hatuwezi kuwepo,” alisema Kaaya.
Alifafanua kuwa kwa miaka zaidi ya minane sasa benki hiyo imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida inayopata kila mwaka kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya sekta za elimu na afya, lakini pia majanga yanayotokea kwa jamii.
Alisema licha ya serikali kujitahidi kuboresha mazingira ya elimu mijini na vijijini, bado ipo haja ya wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo ili kuboresha zaidi mazingira ya kujifunza na kujifunzia.
Walimu wa shule zilizopewa msaada huo wa vifaa vya ujenzi walisema bado zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na kwamba wanafunzi wanasoma kwa zamu, hali inayochangia taaluma na ufaulu duni.
“Ufaulu Kwa kweli siyo mzuri. Mfano mwaka jana, wanafunzi 93 wa Shule ya Msingi Salama A walifanya mtihani wa darasa la nne ambapo waliofaulu ni 40. Kwa Shule ya Msingi Salama B waliofanya mtihani huo walikuwa 113 na waliofaulu ni 58,” alisema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Salama A, Lucas Kaleb.
Aidha, Mwalimu Kaleb alisema kati ya wanafunzi 150 katika shule hizo waliofanya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka jana, waliofaulu ni 61.

Picha ya pamoja.
-------------------------------
Shule za msingi Salama A na Salama B ziko eneo moja zikiwa na wanafunzi zaidi ya 1,500 na vyumba sita vya madarasa sita, na zinakabiliwa na upungufu wa vyumba 21 vya madarasa.
Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda (Vijijini), Mwalimu Deusdedith Bimbalilwa alikiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine katika shule hizo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Barrick yazidi kung’ara mgodi wa North Mara ukitwaa tuzo kwa ulipaji bora wa kodi
>>Serengeti na Ngorongoro: Serikali ya Ujerumani, TANAPA, FZS wazindua miradi ya kijamii iliyogharimu mamilioni ya fedha
>>NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha nne 2024
>>Barrick North Mara yakabidhi bilioni 3.7/- za ‘service levy’ Tarime Vijijini, bilioni 1.7/- za mrabaha kwa vijiji vitano
No comments:
Post a Comment